Subscribe:

search

.

Monday, 6 August 2012

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU KUWEPO KWA MGONJWA WA EBOLA, WILAYA YA KARAGWE MKOA WA KAGERA, TANZANIA

Utangulizi

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa taarifa kwa umma, kuhusu tetesi zilizokuwa zimeenea hapa nchini kutoka kwenye vyombo mbali mbali vya habari kuhusu kuwepo kwa mgonjwa wa Ebola,wilayani Karagwe mkoa wa  Kagera.

Mnamo tarehe 3 Agosti 2012, Wizara ya Afya na Ustawi Wa Jamii ilipokea taarifa kutoka kwa mganga mkuu wa wilaya ya Karagwe ya kuwepo kwa mgonjwa aliyekuwa anahisiwa kuwa na dalili za ugonjwa wa Ebola, katika hospitali ya  Wilaya ya Nyakahanga. 

Aidha,taarifa hiyo ilibainisha kuwa mgonjwa huyo alikuwa ni mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka (6|)  kutoka katika kijiji cha Nyakatundu wilayani Karagwe. Mgonjwa huyu alikuwa na dalili za homa kali, kulegea, kutokwa damu puani, kutapika damu,  na kukojoa damu.

Maelezo kutoka kwa mama mzazi zilieleza kuwa mtoto huyu alianza kuugua kuanzia tarehe 30 Agosti 2012, ambapo alipatiwa dawa ya Septrin baada ya hospitali binafsi kuonyesha kuwa ana  ugonjwa wa“Typhoid”.

Uchunguzi wa awali katika hospitali ya Nyakahanga ulionyesha kuwa mtoto huyu  alikuwa anasumbuliwa na uambukizo kwenye haja ndogo (Urinary Tract Infection).Vile vile alifanyiwa uchunguzi wa kimaabara na Vipimo vya malaria, Hepatitis na Typhoid havikuonyesha kuwepo  kwa magonjwa haya. Hospitali inaendelea kumpatia matibabu mtoto huyu na imewaweka mgonjwa na mama yake anayemtunza kwenye chumba maalum (Isolatiom room) kwa ajili ya uangalizi zaidi. 

Aidha mnamo tarehe 4 Agosti 2012, timu za wataalamu kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na timu ya mkoa wa Kagera imeweza kufika na kumfanyia uchunguzi wa kina pamoja na kuchukua sampuli za damu kwa ajili ya uchunguzi zaidi katika maabara ya Taifa ya uchunguzi wa magonjwa na Maabara za nje ya nchi, ili kubaini kama ameathirika na ugonjwa wa Ebola. 

Timu hiyo ya wataalamu imetoa taarifa kuwa hali ya mgonjwa huyu kwa sasa imeimarika ikiwa pamoja na kutokuwa na homa, kutapika na kukojoa damu kumekoma pia, uchunguzi uliofanywa kwa mama wa mtoto umeonyesha kuwa hana dalili zozote za ugonjwa wa Ebola.Vile vile hakuna taarifa ya mtu mwingine yeyote kwenye familia hiyo au kwenye maeneo ya kijiji hicho au cha jirani kuwa na dalili za ugonjwa huo.

Kufuatia taarifa hii, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na Mkoa wa Kagera imechukua hatua zifuatazo;

Imepeleka timu ya wataalamu mbali mbali kutoka Wizarani na mkoa  kwa lengo la kwenda kufuatilia na kutoa taarifa kuhusu kuwepo kwa ugonjwa huo. 
Imetoa elimu ya Afya kuhusu njia za kuzuia kuenea ugonjwa wa Ebola  pamoja na dalili za ugonjwa huu, kwa wananchi na watumishi wa afya katika hospitali ya Nyakahanga
Kupeleka vifaa kinga katika hospitali ya Nyakahanga pamoja na maeneo ya mipakani
Kutoa matangazo kwa jamii kwa kutumia vipaaza sauti na kupitia  radioni (Radio Karagwe) kuhusu ugonjwa huu.  Aidha, vipeperushi pia vimetolewa.

Hitimisho

Wizara inapenda kuufahamisha umma kuwa mpaka sasa hakuna mgonjwa yeyote aliyethibitishwa kuwa na ugonjwa wa Ebola hapa nchini.Aidha, Wizara ya Afya imejiaanda kikamilifu kukabiliana na ugonjwa huu iwapo utatokea hapa nchini.

Kwa sasa timu za wataalum  zipo katika mikoa ya Mara, Mwanza, Kagera, Kigoma, Kilimanjaro na Arusha, kutoa elimu juu ya ugonjwa huu kwa wataalamu na kwa wananchi na vilevile kufuatilia ugonjwa huu sehemu za mipakani.

Wizara inaendelea kutoa wito kwa wananchi kutoa taarifa haraka kwenye kituo chochote cha kutolea huduma za afya, mara wanapoona dalili za ugonjwa huu.

Imetolewa na:
 kitengo cha Mawasiliano 
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii
Tarehe 6 Agosti, 2012.

JERRY SILAA NAYE AJITOSA VCCM

Mstahiki Meya wa manispaa ya Ilala Jerry Silaa akirejesha  fomu za kugombea nafasi ya ujumbe wa UVCCM-NEC katibu wa UVCCM mkoani Mwanza. Bw. Elias Mpanda, katika ofisi za CCM mkoani- Jijini Mwanza. Mstahiki meya Manispaa ya Ilala Bw. Jerry Silaa anagombea nafasi ya ujumbe wa UVCCM-NEC ngazi ya taifa.
Mstahiki meya  aliweka wazi nia yake ya kutaka kuwawakilisha vema vijana wa kitanzania kwenye UVCCM-NEC na aliwaasa vijana wengine kushiriki kwenye mchakato huo na huku akisisitza kwamba yuko tayari kufanya kazi kokote nchini kwa maslahi ya wananchi, vilevile meya aliwaasa viongozi wote kuwajibika na kutimiza ahadi zao walizozitoa kwa wananchi na kwa kuweka  mbele maslahi ya taifa na sio yao binafsi.

MAKAMU WA RAIS AANDAA FUTARI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiswali na wageni wake na waumini wa dini ya Kiislamu wakati wa hafla ya futari, iliyoandaliwa na Makamu Ikulu Ndogo mjini Dodoma jana, Agosti 5, 2012. Picha na Muhidin Sufiani-OMR

Sunday, 5 August 2012

ANTHON MAVUNDE AJITOSA UVCCM

Mwanasiasa machachari Anthon Mavunde ambaye ni mwenyekiti wa UVCCM Dodoma amejitosa kuwania nafasi ya makamu mwenyekiti wa UVCCM taifa.

CHADEMA SASA KUANZA OPARESHENI SANGARA MOROGORO TAREHE 8


VIONGOZI, POLISI WAKUBALIANA UFANYIKE AGOSTI 8 KILOSA, FFU WAMWAGWA MITAANI KUDHIBITI WAFUASI
Venance George, Morogoro
BAADA ya mvutano wa siku mbili baina ya Jeshi la Polisi na Chadema kilichopanga kufanya mkutano mjini Morogoro jana, pande hizo mbili zilikubaliana kuwa mkutano wa kwanza ufanyike Agosti 8, mwaka huu Mikumi, wilayani Kilosa.
Makubaliano haya yanakuja kufuatia mazungumzo baina ya viongozi wa Jeshi la Polisi mkoani Morogoro na wale wa Chadema kuwa, kwa vile maonyesho ya Nanenane mkutano huo usongezwe mbele na ufanyike wilayani Kilosa Agosti 8, mwaka huu.
Awali Jeshi la polisi lilizuia kwa madai kutokana na kuwapo mgomo wa walimu nchini ambao ulisitishwa kwa amri ya mahakama Alhamisi iliyopita pamoja na kwamba, jeshi hilo halitakuwa askari wa kutosha na kusimamia matukio hayo.
Hata hivyo, kabla ya kufikiwa makubaliano jana hayo askari wengi wakiwagwa mitaani kudhibiti wafuasi wa Chadema kuandamana na kufanya mkutano wa hadhara.
Wakiwa na mabomu ya kutoa machozi, magari yenye maji ya kuwasha, silaha za moto na virungu, vikosi hivyo vilikabiliana na baadhi wafuasi hao kwenye mitaa mbalimbali mjini hapa na kufanikiwa kuwatia nguvuni baadhi yao.
Hali hiyo ilitokana na wafuasi hao kumiminika kwenye ofisi za Chadema mjini hapa kwa ajili ya kuandaa maandamano hadi kwenye Viwanja ambavyo walitarajia kufanyia mkutano wa hadhara.
Wafuasi hao wa Chadema pamoja na viongozi wa ngazi mbalimbali walishiriki kwenye vuguvugu hilo ambalo chama kimelipa jina Vuguvugu la Mabadiliko (M4C), licha polisi kutoa onyo kuwa wasithubutu kufanya maandamano na mikutano hiyo, kwa kile walichodai ni kutokuwa na askari wa kutosha wa kutoa ulinzi.
Jana asubuhi, Jeshi la polisi lilitawanya askari wake kwenye mitaa mbalimbali ya Mji wa Morogoro na barabara zote za kuingia na kutoka katika mji huo.
Magari yenye maji ya kuwasha pamoja na yale yaliyopakia askari wa FFU, yalionekana yaranda randa katika mitaa ya Mji wa Morogoro huku yakipeperusha bendera za rangi nyekundu kuashiria hali ya hatari.
Taarifa zilizopatikana mjini hapa zilidai kuwa vikosi hivyo vya askari zaidi ya 200 waliletwa hapa kutoka mikoa ya Dodoma na Dar es Salaam na kuungana na wenzao wa Morogoro.
Hata hivyo, hali hiyo haikuwaogofya wafuasi na wapenzi wa Chadema, kwani walionekana wakiendelea na maandalizi ya kujikusanya huku wengi wao wakiwa wamevaa sare na kubeba bendera za chama hicho.

Wafuasi hao walionekana wakiwa katika makundi kwa makundi wakielekea kwenye ofisi za wilaya za Chadema zilizoko Mtaa wa Kingo.
Hali hiyo iliwafanya baadhi ya polisi waliokuwa katika mitaa mbalimbali kuanza kuwakamata baadhi yao hususan pale walipoonekana kuwa katika makundi makubwa.
Kitendo hicho kiliibua jazba na kuwafanya baadhi ya wafuasi kutoa maneno makali ya kulilaani jeshi hilo.
Hali hiyo ilionekana kuwatia zaidi hamasa wafuasi hao ambao waliendelea kujikusanya kwa kwenye ofisi za chama huku wakihimiza kuwa waandamane na ikiwezekana wakabiliane na yeyote atakayewazuia.
Kutokana na sakata hilo,  polisi liliomba kukutana na viongozi wa Chadema wa mkoa na taifa ili kujadiliana nao.
Akizungumza na wafuasi na wanachama walifulika katika ofisi hizo baada ya majadiliano na polisi, Mkuu wa Operesheni za Chadema, Singo Benson Kigaila alisema kuwa, Jeshi la Polisi limewaomba kukubali kubadilisha ratiba na kupanga nyingine kadri chama hicho kitakavyopendekeza.
Aliongeza makubaliano yatakwenda sambamba kuwachia huru bila masharti wafuasi zaidi ya 10 walikuwa wamekamatwa pamoja na magari ya chama  hicho.
Alisema Jeshi la polisi limeomba maandamano na mkutano huo uliopangwa kufanyika jana usitishwe kupisha shughuli za maonyesho ya wakulima  ya Nane Nane, Kanda ya Mashariki  yanayofanyika kwenye viwanja vya Mwalimu Nyerere, mkoani hapa.

Alisema kuwa, kufuatia makubaliano hao waruhusiwa kufanya uzinduzi M4C kuanzia Jimbo la Mikumi, wilayani Kilosa Agosti 8 mwaka huu na kuendelea katika majimbo mengine tisa yaliyosalia.
Hata hivyo, Chadema imepanga kufanya mkutano mkubwa katika Jimbo la Morogoro mjini ambao utawahusisha viongozi wa kitaifa na wabunge Agosti 18, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Chadema, maandamano hayo yatapambwa na watembea kwa miguu waliobeba mabango yenye ujumbe mbalimbali.www.mwananchi.co.tz

Karibu Mbogamboga!

Sokoni Morogoro

Alizeti Ni Mafuta Murua

Saturday, 4 August 2012

MKUTANO WA CHADEMA MOROGORO WAZUIWA NA POLISI

Taarifa za uhakika ambazo  Habari Tanzania imezipata kutoka Morogoro ni kuwa polisi wamezuia kabisa mkutano wa chadema,wamemwaga maaskari mamia na sasa kikao cha viongozi wa chadema kinaendelea kuona nini kifanyike. tuone kitakachofuata.

RAIS KIKWETE AFUNGUA WARSHA DODOMA

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akifungua warsha kuhusu mfumo wa kusimamia utekelezaji wa mipango ya maendeleo kwa mawaziri, makatibu wakuu na wakuu wa taasisi za serikali leo Agosti 4, 2012 katika ukumbi wa St Gaspar mjini Dodoma 
Picha na IKULU

NBS YATOA HALI YA UCHUMI


Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Morrice Oyuke akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuelezea hali ya Ukuaji wa Pato la Taifa kwa 7.1% katika kipindi cha robo mwaka 2012.
Picha na Aron Msigwa - MAELEZO.
 OFISI YA TAIFA YA TAKWIMU YATOA TAARIFA YA HALI YA UCHUMI , PATO LA TAIFA LA TANZANIA  LAKUA.
Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
3/8/2012. Dar es salaam.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imetoa taarifa ya hali ya uchumi nchini na kufafanua kuwa  pato la taifa  la Tanzania limekua kwa  asilimia 7.1 katika kipindi cha robo ya mwaka 2012  ikilinganishwa  na asilimia 6.1  za mwaka jana.
Ukuaji huo wa asilimia 7.1 unatokana na ongezeko la uzalishaji katika shughuli mbalimbali za kiuchumi zikiwemo za kilimo, Uvuvi, Viwanda, Ujenzi na zile za utoaji wa huduma mbalimbali za jamii.
Akitoa taarifa hiyo leo jijini Dar es salaam Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Morrice Oyuke amesema kuwa lengo la  utoaji wa taarifa hizo kwa vipindi vifupi vya vya  robo mwaka unalenga kuwapatia wadau wa Takwimu za Pato la Taifa uwezo wa kutathmini mabadiliko ya ukuaji wa uchumi nchini.  
Amesema kuwa jumla ya thamani ya pato la Taifa katika kipindi cha robo ya mwaka 2012 ni shilingi 4,220,535 milioni ikilinganishwa na kiasi cha shilingi milioni 3,940,261 za mwaka 2011.
Amefafanua kuwa ukuaji wa shughuli uzalishaji katika shughuli za kilimo nchini ulifikia asilimia 1.4 katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2012 zikilinganishwa na asilimia 1.2 katika kipindi hicho kwa mwaka 2011 kutokana na upatikanaji wa mvua za kutosha nchini katika mikoa inayozalisha mazao kwa wingi.
 Amesema ukuaji katika shughuli za uvuvi ulikua  asilimia 2.6 katika robo ya kwanza ya mwaka 2012 huku shughuli za uchumi katika sekta ya viwanda na Ujenzi ambayo inahusisha uchimbaji wa madini na kokoto ikikua kwa asilimia 14.3 ikilinganishwa na 0.8% za mwaka 2011.
Bw. Oyuke ameongeza kuwa ongezeko hilo  la uzalishaji wa madini ya dhahabu linatokana na uzalishaji wa wa madini ya dhahabu kutoka kilo 8,140 kwa mwaka 2011 hadi kufikia kilo 16,736 kwa mwaka 2012.
Pia amebainisha kuwa  shughuli za utoaji wa huduma za biashara za jumla na rejareja, ukarabati wa magari na pikipiki na vifaa vingine vya majumbani katika kipindi hicho zilifikia asilimia 9.0 huku shughuli za upangishaji nyumba na biashara zikiwa 8.2 %, uchukuzi na mawasiliano 16.4%, hoteli na migahawa 3.8%, Benki asilimia 15 shughuli za uendeshaji  serikali 6.4%, Elimu 6.1% na utoaji wa huduma za Afya nchini zikikua kwa kasi ya asilimia 5.1.

Friday, 3 August 2012

CWT Wasitisha Mgomo Wa Walimu

 
Chama Cha Walimu Tanzania-CWT-kimetangaza kusitisha rasmi mgomo wa walimu na hivyo kuwataka walimu wote nchini kurejea kazini mara moja kuanzia leo ili kutekeleza majukumu yao ya kila siku kama kawaida.
Akitoa tamko la CWT kwa waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam ikiwa ni siku moja baada ya Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi kukiagiza Chama hicho kitoe maelekezo kwa wanachama wake kurudi kazini, Rais wa Chama hicho GRATIAN MUKOBA amesema walimu wanarudi kazini wakiwa wamekata tamaa kutokana na hukumu hiyo.

Amefafanua kuwa walimu wanaporudi kazini bila kuwa na mawazo yaliyotulia, utendaji wao utaathirika hivyo Chama kinatoa wito kwa Serikali kukutana na CWT kwa haraka ili kuendeleza majadiliano ya Madai mapya ya Walimu.

Kuhusu kulipa fidia ya hasara waliyoipata wanafunzi, Chama hicho kimesema kinasubiri taarifa rasmi ya Serikali kuhusu hasara hiyo kwa kuwa hakina uwezo wa kufahamu hasara waliyoipata wanafunzi.

Kwa mujibu wa Mwalimu MUKOBA wenye uwezo wa kuwasilisha hasara hiyo ni mlalamikaji katika kesi hiyo ambaye ni Serikali.

Hapo jana Chama hicho kilipongeza kauli ya Rais JAKAYA KIKWETE yakusema Serikali inajali na kuthamini mchango wa Walimu nchini.

VIJIMAMBO USWAHILINI!

Kijana ambaye hatukupata jina lake baada ya kupata kipigo kwa tuhuma za wizi wa simu,ubungo stand ya mabasi,jana mchana

KAMA NI WEWE UNGETUMA HIYO HELA?

MGOMO WA WALIMU NI BATILI- MAHAKAMA

Kuwa ulikiuka vifungu kadhaa vya kisheria na sasa walimu wameamriwa na mahakama kurudi kazini na kulipa fidia za hasara walizosababisha.

TAARIFA KUHUSU UKAMILISHWAJI WA BLOG YETU KWA WADAU WETU

Habari za Asubuhi wadau wa Habari Tanzania, tunaomba muendelee kuwa wavumilivu kidogo wakati tunakamilisha baadhi ya maswala nyeti kuhusu blog yetu, lakini siku chache zijazo tutaanza kuwaleteeni habari mbali mbali kwa kadri Mungu atakavyo tuwezesha. Mungu ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.