Subscribe:

search

.

Wednesday, 15 August 2012

DR SLAA AFUKUZWA KATIKA NYUMBA YA KULALA ALIPOFIKIA HUKO KILOSA MOROGORO

  
 

Venance George, Mikumi
KATIBU Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, amefukuzwa katika nyumba ya kulala wageni iliyoko ndani ya Chuo cha Ufundi Stadi (Veta), cha Mikumi wilayani Kilosa, Mkoa wa Morogoro kutokana na kile kinachodaiwa kuwa ni sababu za kisiasa.
Tukio hilo lililoambatana na kuzimwa kwa umeme katika mji mdogo wa Mikumi na vitongoji vyake kwa siku nzima, limetafsiriwa na Dk Slaa kuwa ni hila zinazofanywa na CCM kuhujumu operesheni ya Chadema ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) inayoendelea katika wilaya mbalimbali mkoani humo.
Dk Slaa aliwasili chuoni hapo majira ya saa 8.00 mchana akitokea wilayani Ulanga katika Operesheni M4C ikiwa ni mwendelezo wa Operesheni Sangara iliyofanyika katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Baada ya kuwasili katika hoteli ya chuo hicho, Dk Slaa alipokewa na wahudumu wa hoteli hiyo na kukabidhiwa funguo ya chumba namba tano ambacho Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare, alikiomba kwa ajili yake.
Muda mfupi baada ya kuchukua funguo hizo, akatokea meneja wa hoteli hiyo ambaye jina lake halikufahamika mara moja na kumweleza Dk Slaa kuwa sehemu hiyo imeshawekewa ‘booking’ hivyo Dk Slaa aondoke.
Tukio hilo lilimfanya Dk Slaa ahoji mantiki ya hatua hiyo hasa, baada ya mhudumu wa hoteli hiyo kumkubali na kukabidhi funguo kwake na meneja huyo kumnyang'anya funguo hiyo.
Funguo ya chumba alichotakiwa afikie Dk Slaa alikabidhiwa Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Rwakatare baada ya kukiomba chumba hicho siku kadhaa nyuma.
Hata hivyo, meneja huyo alisisitiza Dk Slaa kuondoka kwa kuwa yeye hakuwa na taarifa na ujio wake.
Kufuatia tukio hilo Dk Slaa aliondoka na kuelekea katika eneo la mkutano wa hadhara ambako pia umeme ulizimwa ghafla hivyo, kuongozea hisia kwa Dk Slaa kuwa alikuwa anahujumiwa kwa kuwa hakukuwa na ratiba ya mgawo wa umeme siku hiyo.
Akizungumza katika mkutano wake huo, Dk Slaa alikituhumu CCM kuwa ndiyo kilichoandaa mpango huo kwa lengo la kuhujumu kampeni zake za kumkomboa Mtanzania.
Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipuuza madai hayo ya Dk Slaa akisema, "Namshauri aache siasa kwa kuwa zimeanza kumshinda,"
Nape alisema Dk Slaa hawezi kueleweka kukihusisha CCM na kufukuzwa kwake hotelini kwani hoteli hiyo ya Veta, siyo mali ya chama hicho tawala.
"Dk Slaa amezeeka. Aache siasa awaachie vijana. Yeye afukuzwe huko halafu aseme CCM tunamhujumu! Namshauri apumzike siasa awaachie vijana waendeleze gurudumu," alisema Nape.
Meneja wa Tanesco, Mkoa wa Morogoro, Deogratius Ndamugaba, akijibu shutuma za kukatika kwa umeme katika mji huo alisema kuwa kukatika huko kulitokana na hitilafu za kawaida na siyo hujuma au msukumo wa kisiasa.
“Kukatika kwa umeme Mikumi si kwa sababu ya Chadema ila ni feeder ya Mikumi iko nje tangu saa 12.45 jioni, nguzo imeanguka na inapaswa kubadilishwa na sehemu yenyewe ni porini, kuna giza na chui,” alisema meneja huyo.

Slaa amvaa Nape
Katika hatua nyingine, Chadema kimemtaka Mwenyekiti wa
CCM, Rais Jakaya Kikwete kutoa elimu kwa viongozi wa chama hicho tawala kuzungumza kwa busara mbele ya wananchi kwani kinyume chake wanamletea sifa mbaya.

Akizungumza katika mikutano ya hadhara ya chama hicho katika vijiji mbalimbali vya Wilaya ya Ulanga, mkoani Morogoro, Dk Slaa alisema kuwa ni kawaida ya mtu mwenye tabia mbaya kama vile mwizi kujishtukia na kufikiria kuwa hata wenzake ni wezi.

Alisema kuwa ni aibu kwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete kuachia viongozi walio chini yake ndani ya chama hicho kutoa matamko yanayoivua nguo Serikali kuwa haiko makini na inazidi kukupoteza dira na mwelekeo wake.

“Nataka nimalizie na suala moja ambalo limetokea leo mchana. Kuna tamko moja limetolewa na kijana mmoja wa CCM anaitwa Nape, sasa kwa sababu ni kama kinda la njiwa kwangu, sitamjibu yeye. Alichokisema kwa watu wanaojua, tunamshangaa Kikwete kwa kuachia mambo ya chama chao na Serikali yake kwa jumla.
Chanzo:Mwanachi.co.tz

0 comments: