Subscribe:

search

.

Tuesday, 21 August 2012

MJUE ALIYEKUWA WAZIRI MKUU WA ETHIOPIA MELES ZENAWI ALIYEFARIKI DUNIA JUZI USIKU


Waziri Mkuu wa Ethiopia, Meles Zenawi
Mwandishi Wetu, Addis Ababa
WAZIRI Mkuu wa Ethiopia, Meles Zenawi (57), amefariki dunia juzi usiku mjini Brussels, Ubelgiji alikokuwa akitibiwa.Taarifa iliyotangazwa na Televisheni ya Taifa ya Ethiopia, imeeleza kuwa Zenawi alifariki dunia saa 5:15 usiku.

Kutokana na Katiba ya nchi hiyo, nafasi ya kiongozi huyo mwenye historia ya kipekee nchini humo, itashikiliwa na Naibu Waziri Mkuu, Hailemariam Desalegn.

Mpaka anakutwa na mauti, hakuna taarifa zozote ambazo zilithibitisha hasa ugonjwa uliosababisha kifo chake. Kiongozi huyo alikuwa madarakani tangu mwaka 1991 alipompindua Mengistu Haile Mariam.
Hata hivyo, taarifa ambazo hazijathibitishwa zinaeleza kuwa Zenawi alikuwa akisumbuliwa na uvimbe kwenye ubongo. 

Habari kwamba kiongozi huyo wa zamani wa vita ya msituni alikuwa mgonjwa, zilianza kusambaa tangu aliposhindwa kuhudhuria mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika, Addis Ababa mwezi uliopita.
Tangu kipindi hicho, wasiwasi ulitanda nchini humo hasa alipochukua likizo. Uvumi huo ulipingwa na Msemaji wa Serikali ya Ethiopia, Bereket Semon ambaye amekuwa akirejea kauli yake hiyo ya kupinga uvumi mara kwa mara.

Msemaji huyo amekuwa akisisitiza kuwa afya ya kiongozi huyo haikuwa mbaya kama ilivyokuwa ikidaiwa na kusisitiza kwamba alichukua likizo baada ya kupewa ushauri na daktari.
Zenawi atakumbukwa kwa sera yake ya kiutawala ambayo ilijulikana kama ‘shirikisho la makabila,’ iliyoyafanya makabila mbalimbali ya nchi hiyo kujitawala yenyewe, lakini bado utawala wake uliendelea kuwa na nguvu.

Zenawi alikuwa mwanasiasa mjanja ambaye aliipenda siasa tangu akiwa kijana mdogo. Alitokea kwenye kundi maarufu la TPLF, ambalo lilikuwa likiongoza mapambano dhidi ya utawala wa kijeshi wa Ethiopia miaka ya 1970 na 1980.

Kiongozi huyo aliyeacha watoto watatu, aliwahi kutajwa kama mmoja wa viongozi wenye ushawishi mkubwa na ambaye utawala wake ulikumbwa na utata barani Afrika.

Wakati Zenawi anafariki dunia, Naibu Waziri Mkuu, Desalegn alikuwa katika mkutano China.
Katika hatua nyingine, Serikali ya Ethiopia ilisema kwamba haitafanya uchaguzi kwa kuwa viongozi waliopo wako imara.

Simon alisema kwa sasa Serikali inashughulika na mazishi ya kiongozi huyo na kwamba mwisho wake wa kuwa madarakani kwa mujibu wa katiba ni mwaka 2015.

“Hakuna wasiwasi wowote na uongozi uliopo madarakani kwani chama kilichopo madarakani kipo katika hali nzuri na kina viongozi imara,” alisema.
Chanzo:www.mwananchi.co.tz

0 comments: