ALIYEKUWA Waziri wa Fedha katika Serikali ya Awamu ya Tatu, Basil Mramba, amesema kutokana na mkataba uliosainiwa na Gavana wa Benki Kuu (BoT), Dk. Daudi Balali na Kampuni ya Alex Stewart, hakuwa na njia yeyote ya kukwepa kuondoa kodi kwa kampuni hiyo.
Mramba pia aliieleza mahakama kuwa, alipokea barua iliyotoka kwa Katibu wa Rais Benjamin Mkapa kwenda kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na nakala iliyokwenda kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati huo, Andrew Chenge, ikiwataka kutafuta fedha za haraka kwa ajili ya kuilipa kampuni hiyo.
Hayo aliyaeleza jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu, John Utumwa, wakati akitoa utetezi katika kesi ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 11.7, inayomkabili yeye na wenzake wawili.
Mramba alieleza kuwa, mkataba uliotiwa saini kati ya BoT na kampuni hiyo ulikuwa unambana kwa mujibu wa sheria ya mkataba huo kwani asingetoa msahama wa kodi, serikali ilitakiwa kumlipa fedha nyingi mwekezaji huyo.
Akiongozwa na wakili wake, Hulbert Nyange, aliyetaka kujua kama maagizo hayo yote aliyachukuliaje kama Waziri wa Fedha, Mramba alidai kuwa yalitolewa na Rais Mkapa katika dokezo mbalimbali akitaka utekelezaji wa kuilipa kampuni hiyo ufanyike haraka iwezekanavyo.
“Mimi sikuruhusu malipo yoyote wala punguzo lolote ila kwa mujibu wa kifungu cha 4 (3), kinasema malipo yoyote hayatatozwa kodi kwa mujibu wa mkataba huo kati ya BoT na Kampuni ya Stewart,” alidai Mramba.
Wakili Nyange alitaka kujua kama ni kweli Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) walitoa ushauri kwa Wizara ya Fedha kuwa wasitoe msahama huo, ambapo alidai kwamba hakuuona ushauri huo.
Aliongeza kuwa yeye hakupaswa kupewa ushauri na TRA, bali kupewa na katibu wake ingawa alikiri kuwahi kuona barua kutoka TRA baadaye, japokuwa ilikuwa imechelewa kwa muda wa siku kumi wakati yeye akiwa ameshaondoa kodi kwa kampuni hiyo.
“TRA hata wangeshauri kwa mujibu wa maagizo niliyoyapata, ingekuwa kazi bure, kwanza walishachelewa. Na hata hivyo tangu kupata Uhuru, sheria inatoa mamlaka kwa waziri wa fedha kusamehe kodi ilimradi msahama huo uwe na manufaa kwa wananchi wake bila kushauriana na mtu yeyote,” alidai Mramba.
Alipoulizwa kuwa inadaiwa alikurupuka baada ya kulala nyumbani kwake na asubuhi akaandika dokezo kwa serikali la kuondoa kodi hiyo, Mramba alisema hakufanya hivyo bali Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliagiza kufanya hivyo na kwamba yeye alitekeleza maagizo hayo.
Mramba, Daniel Yona aliyekuwa Waziri wa Fedha na aliyekuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Grey Mgonja, walifikishwa mahakamani mwaka 2008 wakidaiwa kuwa kati ya Agosti 2002 na Juni 14, 2004, Dar es Salaam, washtakiwa wakiwa watumishi wa umma, walitumia vibaya madaraka yao na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 11.7.
Ilidaiwa kuwa washtakiwa hao waliipatia msamaha wa kodi isivyo halali, Kampuni ya M/S Alex Stewart ya Uingereza. Kesi hiyo imehairishwa hadi Oktoba 12 mwaka huu, ambapo Mramba ataendelea kutoa ushahidi wake mahakamani hapo.
Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment