SERIKALI imetenga Sh326 bilioni kwa ajili ya kugharimia mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi 98,772 katika kipindi cha mwaka wa fedha 2012/13.Idadi hiyo ya wanafunzi ni ongezeko la takriban wanafunzi 5,596 ikilinganishwa na wanafunzi 93,176 waliopata ufadhili wa bodi hiyo mwaka jana. Hayo yalielezwa jana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa wakati akisoma Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2012/13. “Katika mwaka 2012/13, wizara kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, itatekeleza yafuatayo; kutoa mikopo kwa wanafunzi 98,772 wa vyuo vya elimu ya juu na kusimamia ukusanyaji wa marejesho ya mikopo ya Sh18 bilioni kwa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wadaiwa,’’ alisema Dk Kawambwa. Waziri alisema kati ya wanafunzi 93,176 waliopata mikopo kwa kipindi cha mwaka wa fedha uliopita, 256 walikuwa wahadhiri ambao walikuwa wakisomea shahada za uzamili na uzamivu ndani na nje ya Nchi. Alisema katika mwaka huu wa fedha, Wizara inakusudia kudahili wanafunzi 65,000 wanaojiunga na vyuo vikuu kama hatua za kufikia lengo la wanafunzi 300,000 kwenye Taasisi ya Elimu ya Juu ifikapo mwaka 2015. Alisema mipango mingine ni kuanza mchakato wa ujenzi wa ofisi za bodi ili kuongeza ufanisi katika kazi na kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu wajibu wa kuchangia elimu ya juu na urejeshaji wa mikopo. Waziri alisema Wizara yake inaendelea kuongeza ufanisi katika usambazaji wa mitihani kwa kununua matrela mawili ya malori na magari madogo mawili kwa ajili ya ufuatiliaji na usindikizaji wa mitihani hiyo. Alisema kupitia Baraza la Mitihani la Taifa, Wizara itasimamia Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi kwa watahiniwa 1,050,000 wanaotarajia kufanya mtihani huo mwaka huu. Katika bajeti hiyo, Waziri Kawambwa aliomba Bunge liidhinishe matumizi ya Sh724.5 bilioni kwenye wizara hiyo kwa mwaka huu wa fedha ikiwamo ni fedha za matumizi ya kawaida, mishahara na matumizi mengineyo. Kamati: Kodi zipitiwe upya Serikali imeshauriwa kupitia upya utaratibu wa kodi zinazotozwa kwa taasisi binafsi za elimu nchini zikiwamo zinazotoa elimu ya msingi na sekondari ili kuzisaidia taasisi hizo kuongeza ufanisi katika utoaji wa elimu. Ushauri huo ulitolewa bungeni jana na Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Martha Mlata wakati akiwasilisha taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii kuhusu Bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa mwaka 2012/13. Mlata alisema watu na taasisi binafsi za elimu nchini zimekuwa zikichangia juhudi za Serikali katika kutoa elimu ya msingi, sekondari na vyuo kwa kuzingatia miongozo ya wizara lakini zinakabiliwa na changamoto kubwa ya kodi. “Taasisi hizi zinakabiliwa na changamoto ya utozwaji wa kodi ikiwamo kodi za ardhi, majengo, mapato, kodi ya kuajiri mwalimu au mfanyakazi asiye raia wa Tanzania hali inayosababisha uendeshaji wa taasisi kuwa mgumu,” alisema. Kamati hiyo pia imebainisha kuwapo kwa mgongano katika utekelezaji wa sera ya uchangiaji elimu hususan utoaji wa elimu ya msingi na sekondari hali inayosababisha baadhi ya wazazi kugoma kuchangia elimu kwa watoto wao. Madai ya Upinzani Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, imeitaka Serikali kuwarudisha vyuoni wanafunzi 285 wa vyuo vikuu waliosimamishwa masomo wakigomea utendaji mbovu wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi Nchini. Msimamo huo uliwasilishwa bungeni jana na Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Susan Lyimo wakati akiwasilisha maoni ya kambi hiyo kuhusu Bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo 2012/13. Kati ya wanafunzi hao, 260 ni wa Chuo Kikuu Dodoma (Udom) na wanafunzi 25 ni wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Chanzo:Mwananchi |
Monday, 13 August 2012
SERIKALI IMEONGEZA IDADI YA UDAHILI WA WANAFUNZI KATIKA VYUO VIKUU
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment