Subscribe:

search

.

Monday, 13 August 2012

WAKULIMA WA KOROSHO MKOANI PWANI WAITAKA SERIKALI IWALIPE MADENI YAO 23M VINGINEVYO WATAGOMA KUHESABIWA KWENYE SENSA



Wakulima wa korosho wa Kijiji cha Ndundu Tawa Wilaya ya Rufiji Mkoani Pwani wamesema hawapo tayari kuhesabiwa katika zoezi la sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika nchini kote kuanzia august 26 mwaka huu iwapo serikali haitasaidia wakulima hao kulipwa madai yao ya zaidi ya shilingi zaidi ya milioni 23.

Akizungumza na Uhuru Fm mwenyekiti wa wakulima wa korosho kijijiji cha Ndundu Tawa ndugu JUMANNE SUDI amesema anaomba serikali iingilie kati ili wapewe haki yao kama ilivyoingilia kati kudai madai ya baadhi ya wakulima katika mikoa mingine ya kusini.

Ndugu SUDI amesema pia wakulima hao wana mpango wa kuandamana hadi kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda ili kufikisha ujumbe wao kutokana na kile walichosema kukosa imani na uongozi wa ngazi za chini hasa kutotekeleza agizo la Serikali  juu ya kutatua kero zao jambo linalosababisha kukosa haki zao za msingi.

Wakazi hao wapatao 30 ambao ni wakulima wa zao la korosho wamesema kuwa wamefikia hatua hiyo baada ya kuwa wavumilivu wa muda mrefu juu ya kudai pesa zao kiasi cha shilingi milioni 23 kutoka katika chama cha msingi cha Chumbi chenye makao yake makuu katika Kijiji cha Ndundu tawa ambayo ni malipo ya mauzo ya korosho.

Wakizungumza na waandishi wa habari kwa masikitiko wakazi hao walisema  hivi sasa wamepoteza imani kama watapatiwa pesa zao hizo wanazokidai chama cha ushirika kutokana na kuwa kipindi kirefu kimepita na wanapokwenda kudai pesa zao viongozi wa chama hicho wamekuwa wakiwapiga chenga huku wakishindwa kuwapa majibu ni lini watawalipa.

Wakizungumzia juu ya kuandaa maandamano walisema kuwa mapema mwaka huu Waziri Mkuu alipokuwa akizungumzia juu ya madai ya wakulima kwa vyama vya ushirika vya msingi kupitia vyombo vya habari alisema kuwa Serikali imetoa pesa kwaajili ya kuvikopeshavyama vyote vya msingi ili viwalipe wakulima wa korosho lakini wanachoshangaa ni wao kutolipwa mpaka sasa wakati katika maeneo mengine malipo yameshafanyika.

“Waziri Mkuu alitangaza kupitia vyombo vya habari kuwa Seriklai imevikopesha vyama vya msingi nchini kote ili viwalipe wakulima madeni yao ya korosho kwa msimu huu uliopita na kuna baadhi ya mikoa wenzetu wamelipwa sasa kwetu hakuna hata dalili yoyote ya kulipwa” Alisema Mmoja wa wakulima hao aliyejitambulisha kwa jina la Jumanne Sudi.

Wameongeza kuwa kutokana na hilo hawaoni umuhimu wa wao kuhesabiwa katika zoezi la Sensa ya watu na makazi kwani kama Serikali haikuwajali kabla hawajahesabiwa hivyo hatakama watahesabiwa hakutakuwa na manufaa yoyote watakayoyapata.

Akijibu juu ya malalamiko hayo Mwenyekiti wa Chama cha msingi cha Chumbi Juma Mikole amekiri kuwepo kwa deni hilo na kubainisha kuwa hali hiyo imetokana na kukosekana kwa soko la korosho nchini  ambapo alisema kuwa katika kuhakikisha wanawalipa pesa zao wametoa ombi kwa Serikali ili kusaidia upatikanaji wa mnunuzi wa zao hilo kwa wakati.

Mwenyekiti huyo amewataka wakulima hao kuwa na subira kwa kipindi hiki ambapo wanalishugulikia suala lao na kubainisha kuwa hakuna atakayedhurumiwa pesa zake pindi watakapokuwa wameziuza korosho hizo.
Chanzo:www.blogzamikoa.blogspot.com

0 comments: