WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewataka wakulima wa mpunga nchini kuanza kujipanga kuuza mchele nje ya nchi. Pinda alisema hayo juzi wakati akikagua kazi ya kuweka mitambo ya kinu cha kukoboa mpunga katika kata ya Mwamapuli na Majimoto wilayani Mlele mkoani Katavi, na ujenzi wa madaraja ya mto Msadya na mto Kavuo. Aliendelea kusema kuwa kulingana na mahitaji yatakayokuwepo, wakulima hao kama watajipanga vizuri wanaweza kuuza mchele watakaouzalisha hadi katika nchi za Burundi na Rwanda ambako soko la uhakika lipo. “Kwa mahitaji yatakayokuwepo, na kama wakulima watajipanga vizuri wanaweza kuuza mchele mpaka nchi za Rwanda na Burundi,” alisema Pinda kwenye taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na ofisi yake. Aliendelea kufafanua kuwa kukamilika kwa mradi huo kutawasaidia wakulima kuuza mchele badala ya kuuza mpunga, ndipo alipoelekea Mwampuli kukagua kinu hicho kilichonunuliwa kwa fedha za Halimashauri kwa lengo la kuwasaidia wananchi wa kata hizo Kwa upande mwingine, diwani wa kata hiyo, Emmanuel Mponda alimweleza Waziri Mkuu kuwa kinu hicho kina uwezo wa kukuboa tani 300 kwa siku kikiendeshwa kwa saa nane kutwa nzima. Diwani huyo alieleza kuwa kinu hicho kina uwezo wa kuchambua mchele na kuupanga katika madaraja manne tofauti na kuufungasha kwa madaraja hayo, na kinatarajiwa kuanza kazi Septemba mara jenereta litakapokamlika kuunganishwa. “Mchele ukishakobolewa, unapangwa katika madaraja A, B, C, na daraja D zinakuwa ni chenga ambazo zitauzwa peke yake kwa ajili ya wauza vitumbua. Kinu hiki pia kina uwezo wa kutenganisha pumba kwa ajili ya mifugo na kuzipaki katika sehemu ya peke yake bila kuingiliana na uzalishaji wa mchele,” alisema Mponda. Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda Vijijini, Wilbroad Mayala alisema kinu hicho kimegharimu Sh96 milioni wakati jenereta la kuendesha kinu hicho lenye uwezo wa kuzalisha kilowati 120, limenunuliwa kwa sh86 milioni. Chanzo:mwananchi.co.tz |
Monday, 27 August 2012
WAKULIMA WA MPUNGA KATAVI WANUSURIWA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment