Subscribe:

search

.

Saturday, 25 August 2012

Zitto:Kiama walioficha mabilioni Uswisi

Zitto Kabwe
ASEMA ATAFANYA HIVYO BUNGE LA OKTOBA KAMA SERIKALI ITASHINDWA, MABILIONI HAYO YAHUSISHWA NA UFISADI WA MEREMETA
Waandishi Wetu
MBUNGE wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe ameahidi kuwataja wanaohusika kuficha mabilioni ya fedha nchini Uswisi katika kikao kijacho cha Bunge Oktoba, mwaka huu iwapo Serikali itashindwa kufanya hivyo hadi muda huo.
Wakati Zitto akisema hayo, kashfa hiyo imechukua sura mpya na sasa fedha hizo zinahusishwa na ufisadi katika Kampuni ya Meremeta.
Kauli ya Zitto ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, imekuja siku chache tangu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta kuwataka wanaowafahamu walioficha fedha hizo kuwataja hadharani ili iwe rahisi kwa Serikali kuwachukulia hatua.
Hata hivyo, Zitto akizungumza na gazeti hili jana alisema: “Mimi ni mbunge makini ninayefahamu taratibu za Bunge na kuheshimu haki za watu wengine, siwezi kukurupuka katika suala hili. Ninaiachia Serikali na vyombo vyake iendelee kulifanyia kazi na ikiwa watashindwa kuwataja wahusika, basi wasubiri kikao kijacho, nitaweka hadharani majina ya wahusika wote.”
Zitto alisisitiza kuwa Serikali ina uwezo wa kupata taarifa zozote inazozihitaji kutoka Uswisi na kwamba ndiyo maana ameipa muda wa kulifanyia kazi suala hilo kabla yeye hajachukua hatua ya kuwataja wahusika.
“Sikia, lazima tukubaliane jambo moja kwamba mimi siyo Serikali, wala sina dola, ndiyo maana nasema kwamba tusubiri utekelezaji wa ahadi ya Serikali, lakini wakishindwa kuwataja, basi mimi nitatumia nafasi yangu kama mbunge kuwataja na nitafanya hivyo ndani ya Bunge na wala siyo nje ya hapo,” alisema.
Uchunguzi zaidi wa gazeti hili umebaini kuwa kiasi cha Dola za Marekani 186 milioni (takriban Sh300 bilioni) kwa viwango vya sasa vya kubadilishia fedha ambavyo ni Sh1,600 kwa Dola ya Marekani, kimefichwa katika benki tatu tofauti za Uswisi.
Uchunguzi zaidi unabainisha kuwa takwimu hizo ni rasmi kwani zimetolewa na Benki Kuu ya Uswisi, lakini taarifa zaidi zinadai kuwa kuna fedha nyingi zaidi zilizofichwa na Watanzania katika benki nyingine nchini humo ambazo taarifa zake zinaweza kupatikana ikiwa Serikali itasimamia vizuri suala hilo.
Watanzania 27 wameripotiwa kumiliki fedha nchini humo, na mmoja wao anadaiwa kwamba anamiliki Dola za Marekani 56 milioni (wastani wa Sh89.6 bilioni).
Kashfa ya kuwapo kwa vigogo walioficha fedha zao Uswisi iliibuliwa na baadhi ya vyombo vya habari nchini Juni mwaka huu na baadaye mwangwi wake kulitikisa Bunge katika Mkutano wake wa Nane uliomalizika hivi karibuni.
Habari hizo zilikuwa zikinukuu taarifa ya Benki Kuu ya Uswisi iliyoitoa na kuonyesha kuwapo kwa kiasi cha Sh315.5 bilioni zilizotoroshwa Tanzania na kufichwa nchini humo na vigogo ambao ni wanasiasa pamoja na wafanyabiashara.
Suala hilo pia lilijadiliwa katika kikao cha Bunge kilichopita, huku ikidaiwa kwamba fedha hizo zinatokana na biashara (deals) zilizofanywa na watendaji wa Serikali na wafanyabiashara kwenye sekta za nishati na madini na kwamba sehemu kubwa ya fedha zililipwa na kampuni za utafutaji mafuta na gesi katika Pwani ya Mkoa wa Mtwara zilizopewa mikataba kati ya mwaka 2004 na 2006.

Uhusiano na Meremeta

Habari zaidi zinadai kuwa fedha zilizofichwa Uswisi hivi sasa zina uhusiano na ufisadi kupitia Meremeta unaohusisha kiasi cha Dola za Marekani 132 milioni wastani wa Sh211.2 bilioni ambazo zilitoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwenda Benki ya Ned Afrika Kusini.
Fedha hizo zililipwa kama marejesho ya mkopo wa Dola 10 milioni (sawa na Sh1.6 bilioni tu, uliokuwa umechukuliwa na Kampuni ya Meremeta Ltd ambayo ilikuwa mali ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), ikishughulikia uchimbaji wa madini.
Utata katika malipo hayo ni uhalali wa ongezeko la Dola 122 milioni katika malipo hayo, kwani mkopo wa Dola za Marekani 10 milioni ulirejeshwa na faida ya zaidi ya asilimia 1,000.

Uchunguzi unaonyesha kuwa fedha hizo za marejesho tata zilifichwa katika benki moja (jina tunalihifadhi) nchini Mauritius, na baadaye kati ya 2005 na 2006 zilihamishiwa nchini Uswisi, ambako sehemu yake zipo kwenye akaunti ya kigogo ambayo inaongoza kwa kuwa na kiasi kikubwa cha fedha, karibu Sh90 bilioni.
Kashfa ya Meremeta ni ya muda mrefu na mara nyingi Serikali imekuwa ikikataa kuizungumzia kwa maelezo kwamba ni suala ambalo lina masilahi ya usalama kwa taifa.
Awali, Serikali ilisema kwamba Meremeta Ltd ni kampuni ya Kitanzania iliyokuwa ikimilikiwa na JWTZ kwa ajili ya mradi wake wa Nyumbu, Mkoa wa Pwani.
Taarifa za usajili zilizotolewa na Msajili wa Kampuni wa Uingereza na Wales zinabainisha kuwa kampuni hiyo iliandikishwa nchini humo mwaka 1997 na baadaye ilifilisiwa hukohuko Uingereza mwaka 2006.
Taarifa ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) ya Mei 31, 2005 inabainisha kwamba Meremeta Ltd ni tawi la kampuni ya kigeni iliyosajiliwa Tanzania, Oktoba 3, 1997 na kwamba hisa 50 za kampuni hiyo zilikuwa zinamilikiwa na Kampuni ya Triennex (Pty) Ltd. ya Afrika Kusini, wakati hisa 50 zilizobaki zilikuwa zinamilikiwa na Serikali ya Tanzania.
Utata kuhusu umiliki wa Meremeta Ltd unatokana na taarifa ya Brela ambayo pia inazitambua kampuni mbili za Kiingereza ambazo ni London Law Services Ltd na London Law Secretarial Ltd kuwa wamiliki wa hisa moja kila moja ndani ya Meremeta.
Licha ya Serikali kutokuwa mmiliki pekee wa kampuni hiyo, BoT ililipa madeni yote ya Meremeta badala ya kusaidiana na washirika wake ambao kisheria wanaonekana kuwa walikuwa wakimiliki hisa katika kampuni hiyo.
Serikali Tanzania ilikuwa ikimiliki asilimia 50 ya hisa na kwa mujibu wa taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), uhalali wa malipo hayo ulikuwa na walakini kwani kiutaratibu, Nedbank Ltd ilitakiwa iachwe idai fedha zake kutoka kwa mfilisi wa kampuni hiyo kama ilivyo kwa wadeni wengine.

Meremeta bungeni

Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini iliwahi kupewa idhini ya kuchunguza suala hilo, lakini Spika wa Bunge, Anne Makinda alilihamishia katika Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.
Hata hivyo, uchunguzi huo haukuwahi kufanyika na Ofisi ya Spika pia haijawahi kutoa taarifa yoyote. Hivyo suala hilo kubaki kitendawili hadi leo.
Hatua ya Spika kuridhia uchunguzi ilikuja baada ya mvutano wa muda mrefu, uliotokana na hoja zilizokuwa zikitolewa na Serikali kwamba suala la Meremeta lisingeweza kufanyiwa uchunguzi kutokana na “sababu za kiusalama.”
Kumbukumbu za Bunge zinaonyesha kuwa Zitto aliwahi kuwasilisha barua kwa Katibu wa Bunge akitoa taarifa ya hoja ya kutaka kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge kwa ajili ya kuchunguza tuhuma za ufisadi kupitia kampuni hiyo ya uchimbaji wa dhahabu.
Zitto alitoa taarifa ya mdomo bungeni Julai 13, mwaka jana kwa mujibu wa Kanuni ya Bunge Namba 117 (2)-(a) inayomruhusu kutoa taarifa ya kusudio lake la kuwasilisha hoja ya kutaka Bunge liunde kamati teule.
Aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi (sasa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii) aliwahi kusema bungeni kwamba halifahamu suala hilo kwenye majumuisho ya Bajeti ya wizara hiyo ya 2011/12
Chanzo:www.mwananchi.co.tz

0 comments: