NIMECHUKUA HATUA YA KUWASILISHA KWA TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA SUALA LA MATATIZO YA MAJI KATIKA KATA YA GOBA ILI HATUA ZA HARAKA NA ZA KUDUMU ZICHUKULIWE
Kazi
ya mbunge ni kuwakilisha wananchi, kushiriki katika kutunga sheria na kuisimamia
serikali ili kuwezesha maendeleo kwa pamoja na mambo mengine kuhakikisha huduma
za kijamii ikiwemo upatikanaji wa maji zinaboreshwa.
Tarehe 10 Oktoba 2012 ikiwa ni sehemu ya kufanya kazi hiyo nimekwenda
kwa niaba ya wananchi Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na kuwasilisha
malalamiko ya uvunjwaji wa haki za binadamu za kupata huduma ya maji na
ukiukwaji wa misingi ya utawala bora katika uendeshaji wa miradi ya maji kwenye
kata ya Goba katika Manispaa ya Kinondoni.
Tatizo la maji katika kata ya Goba limedumu sasa kwa kipindi cha
miaka mingi kabla ya mimi kuchaguliwa kuwa mbunge, pamoja na kwamba serikali
inaowajibu wa kuhakikisha inalinda haki ya kupata maji lakini Halmashauri ya
Manispaa ya Kinondoni imeshindwa kulinda haki hii kwa wakazi wa Goba.
Ifahamike kuwa miongoni mwa haki za kijamii kwa mujibu wa Mkataba
wa Kimataifa wa Haki za Kiuchumi, Kijamii na Kiutamaduni (“The International
Covenant on Economic, Social and Cultural Rights”, ICESCR ) wa 1966
ni pamoja na haki ya kupata maji safi na salama.
Hata hivyo katika nchi yetu inaonekana haki ya kupata maji safi na
salama haitiliwi mkazo pamoja na Tanzania kutambua na kuridhia mkataba huo hivyo
malalamiko haya ya lengo la kuwezesha tume kusimamia haki za msingi za binadamu
na utawala bora katika sekta ya maji.
Ikumbukwe kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka
1977, toleo la mwaka 2005 Ibara ya 130 (b) na (c) inaeleza majukumu ya Tume ya
Haki za binadamu na utawala bora kuwa ni pamoja na kupokea malalamiko ya
uvunjaji wa haki za binadamu na kufanya uchunguzi juu ya mambo yanayohusu
uvunjaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa utawala bora;
Izingatiwe kuwa Sheria ya Haki za binadamu na Utawala Bora namba 7
ya mwaka 2001 kifungu cha 22(1) kinaruhusu malalamiko kwa njia ya maandishi ;
Na Irejewe kuwa kuwa kifungu cha 15(1) (b) (iii) cha Sheria ya Haki
za Binadamu na Utawala Bora, sheria namba 7 ya mwaka 2001, kinaipa nguvu Tume
kuchunguza uvunjaji wa Haki za Binadamu ikiwa itapokea malalamiko kutoka kwa
mtu anayefanya hivyo kwa niaba ya kundi la watu.
Kwa kutumia mamlaka na matakwa ya Ibara ya 130 ya Katiba ya Nchi na
vifungu vya 15 na 22 vya Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na utawala bora na
kwa kuzingatia mikataba ya haki za binadamu ambayo nchi yetu imeridhia nimetaka
tume ichukue hatua zifuatazo:
Mosi; Ichunguze na kuchukua hatua dhidi ya waliohusika katika
ukiukwaji wa haki za binadamu za wananchi kupata huduma ya maji na ukiukwaji wa
misingi ya utawala bora kwa kushindwa kushughulikia matatizo ya kimfumo kuhusu
uendeshaji wa miradi ya maji, kutokutekelezwa kwa wakati kwa vipaumbele vya maji
kwa mujibu wa bajeti iliyopitishwa na tuhuma za ufisadi, uzembe na udhaifu wa
kiutendaji katika kamati za maji, ngazi ya kata na kwenye idara ya maji ya
Manispaa ya Kinondoni.
Pili; Pamoja na kuchukua hatua kwa wahusika waliosababisha uvunjaji
wa haki ya msingi ya wananchi kupata huduma ya maji na ukiukwaji wa haki za
binadamu; Tume ya Haki za Binadamu ipendekeze hatua za haraka zinazopaswa
kuchukuliwa na Manispaa ya Kinondoni kuwezesha huduma ya maji kurejea kwa
wananchi, kupanua kwa dharura wigo wa upatikanaji wa maji kwa wananchi wa Kata
ya Goba pamoja na kuboresha mfumo mzima wa upangaji, utekelezaji na usimamizi wa
miradi ya maji katika Manispaa ya Kinondoni.
Tatu; Aidha, zaidi ya hatua za dharura Tume ya Haki za Binadamu
ipendekeze hatua za ziada ya kuchuliwa na Manispaa ya Kinondoni kuwezesha kata
ya Goba itoke katika kupatiwa huduma ya maji chini ya Manispaa ya Kinondoni na
badala yake ihudumiwe na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es salaam
(DAWASA) pamoja na Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASCO) ili
kuwezesha uboreshaji mpana wa miundombinu kwa ajili ya ufumbuzi wa
kudumu.
Nne, Tume ichunguze na kupendekeza masuala mengine ya kushughulikiwa
na mamlaka zingine zinazohusika ikiwemo Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji
(EWURA), Wizara ya Maji na Vyombo vya Ulinzi na Usalama kuhusu masuala ya
ukiukwaji wa haki za binadamu na uvunjwaji wa misingi ya utawala bora katika
miradi ya maji kwenye kata ya Goba pamoja mfumo wa upatikanaji wa maji kwa
ujumla.
Wenu katika kuwakilisha wananchi,
John Mnyika (Mb)
12/10/2012
0 comments:
Post a Comment