Uganda ilipata uhuru wake Oktoba 09,
mwaka 1962 na jana Jumanne 09 Oktoba, 2012 iliadhimisha miaka 50 ya uhuru huo
katika sherehe zilizofanyika katika uwanja wa Mapinduzi wa Kololo na
kuhudhuriwa na Mwenyeji wa Sherehe hizo Rais Yoweri Kaguta Museveni.
Sherehe hizo za aina yake zilipambwa na
vikosi mbalimbali vya kijeshi vilivyopita mbele ya Amiri Jeshi Mkuu Rais
Museveni na kutoa heshima zao za utii kwa kiongozi huyo, sambamba na vikundi
mbalimbali vya burudani ambavyo vilitumbuiza wakati wote wa sherehe, huku
wananchi mbalimbali wa Uganda ambao hawakupata nafasi ya kufika katika uwanja
wa Kololo wakitazama tukio hilo la kihistoria kupitia televisheni mbalimbali.
Sambamba na hilo pia vyombo mbalimbali
vya kiusalama, vilikuwa vikitumia kila aina ya taarifa sambamba na kuzunguka
eneo la maadhimisho wakati wote ili kuhakikisha kuwa sherehe hizo zinafanyika
na kumalizika kwa usalama kama ambavyo imetokea.
Sherehe hizi ziliongozwa kwa lugha
tatu, ya kwanza ikiwa ni Kiswahili ambacho kilitumika kutoa amri kwa vikosi vya
majeshi na hii inadhihirisha wazi kuwa lugha hii imejikita zaidi miongoni kwa
wanajeshi wa Uganda, lugha ya Kiganda na Kiingereza.
Vyombo mbalimbali vya habari vya Uganda
vimeelezea kuwa tukio hili la kuadhimisha miaka 50 ya uhuru, ni moja ya matukio
makubwa kabisa ambayo yametokea Uganda na ambayo yameonesha kuwa taifa hilo
lina kila sababu ya kuunganisha nguvu zake na kubakia taifa moja tofauti na
sasa ambapo kuna hali kadhaa za kusigana miongoni mwa wananchi hali inayofanya
kukosekana kwa utulivu wa moja kwa moja.
0 comments:
Post a Comment