Subscribe:

search

.

Thursday, 11 October 2012

WARIOBA: HAKUNA NCHI AMBAYO WANANCHI WOTE WALIANDIKA KATIBA YAO





Na: Matern Kayera

MWENYEKITI wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema hakuna nchi duniani inayotengeneza katiba kwa kuchukua maoni ya kila mwananchi kama wanavyodai baadhi ya watu na asasi za kiraia hapa nchini. Warioba alisema hayo jana jijini Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za Tume hiyo.

 Alisema Tume yake inajitahidi kuwafikia wananchi wengi zaidi ili kupata maoni yenye mitazamo tofauti kwa nia ya kujenga mwafaka wa kitaifa. 

Warioba alisema hayo baada ya waandishi wa habari kutaka ufafanuzi kuhusiana na taarifa iliyotolewa na Jukwaa la Katiba hivi karibuni kuwa kuna hali ya kusuasua katika mchakato unaoendelea wa ukusanyaji maoni kutokna na Tume kuchukua maoni kwenye kata chache huku nyingi zikiachwa. 

Alisema Tanzania ni nchi kubwa na idadi ya watu ni wengi, hivyo kumfikia kila mwananchi aliko kama baadhi ya watu wanavyosema, siyo kitu rahisi. Alisema mpaka sasa Tume inaridhishwa na hamasa waliyonayo wananchi kwa kujitokeza kwa wingi na kutoa maoni yao katika mikutano inayoendelea maeneo mbalimbali nchini. 

 “Jumla ya mikutano 842 imefanyika ambapo jumla ya watu 517,427 walihudhuria. Awamu ya kwanza zaidi ya watu 189,000 walihudhuria na awamu ya pili watu 327,000. Wananchi waliotoa maoni kwa maandishi ni 77,405; waliozungumza ni 29,514.

 Waliotoa maoni kwa njia ya tovuti 3,577 kati yao 12 wanaishi ughaibuni, kwa njia ya mtandao wa facebook 2,338, kwa njia ya barua 2,500 na kwa njia ya magazeti tumepata maoni 670 hadi sasa,” alisema Jaji Warioba.

 Warioba alisema kwamba maoni yaliyotolewa na wananchi ni mengi na yana uzito mkubwa kwani yamegusa maeneo mbalimbali kama vile utawala na maendeleo. Alisema mwamko huu wa wananchi unaonyesha ni aina gani ya utawala wanautaka katika Tanzania.

 Alisema makundi maalumu kama vile wanawake, walemavu na wafungwa pia wamepata fursa ya kutoa maoni yao kwenye mikutano inayoendelea kwa maandishi au kwa kuzungumza. Alisema ushiriki huu wa wananchi kwa makundi mbalimbali utasaidia kupata katiba inayowakilisha wananchi wote. 

 Pia alisema kuwa NGOs zina wajibu wa kutoa elimu na kuhamasisha wananchi ili washiriki kwa wingi katika kutoa maoni yao na siyo kutafuta upungufu tu. Warioba alisema kuwa Tume imepewa miezi 18 kukamilisha kazi ya kuandika katiba Mpya, ila akafafanua kuwa muda unaweza kuongezwa kama kazi haijakamilika. 

Pia aliviomba vyombo vya habari viendelee kuisaidia Tume kwa kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni yao

0 comments: