Subscribe:

search

.

Tuesday, 2 October 2012

HIVI NDIVYO ILIVYOKUWA KATIKA MITAA YA ARUSHA BAADA YA MAHAKAMA KUSIKILIZA RUFANI YA LEMA



 

 Na: Mussa Juma, Arusha,Mwananchi. 

 Aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema akiwahutubia wafuasi wake baada ya Jaji MKuu wa Tanzania Mohamed Chande Othman kuahirisha kesi ya rufaa ya aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema.Picha Zote na Jackson Odoyo Mussa Juma, Arusha MAWAKILI wanaomtetea aliyekuwa Mbunge wa Arusha, Godbless Lema wamedai mbele ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kuwa mteja wao yuko huru kwa kuwa mahakama haikutengua ubunge wake.Katika kesi hiyo, Jaji Mkuu, Mohamed Othman Chande anawaongoza wenzake wa Mahakama ya Rufani, Salum Massati na Natalia Kimaro kusikiliza maombi ya rufani hiyo, inayopinga Lema kuvuliwa ubunge. 

Mawakili hao wa Lema jana walitoa hoja ya kupinga hukumu hiyo kufuatia mabishano baina yao na upande wa utetezi kwa maelezo kuwa taratibu za ufunguaji wa rufaa hiyo zimekosewa. Awali wakili Alute Mughwai aliiomba mahakama hiyo kutupilia mbali rufani hiyo kwa kile alichoeleza kuwa ina upungufu mwingi wa kisheria na kikanuni. Wakili huyo alitaja baadhi ya kasoro za rufani hiyo kuwa ni hati ya kukaza hukumu (tuzo) ambayo imewasilishwa mahakamani hapo kutokuwa na mhuri wa Jaji Gabriel Rwakibarila aliyetoa hukumu ya kesi hiyo. 

 Alidai kuwa katika rufani hiyo pia kuna upungufu kuhusu tarehe za kuwasilishwa kwa rufani, pia baadhi ya vifungu vimekosewa.Wakili Mughwai alitoa kumbukumbu ya kesi kadhaa ambazo mahakama ya rufani ilizitupa baada ya kukosa hadhi ya kisheria kusikilizwa.

 “Mawakili wa Lema walipaswa kabla ya kuwasilisha mahakamani rufani yao, kujiridhisha kama kuna upungufu katika nyaraka ambazo wanawasilisha mahakamani.” Alisema kubwa katika makosa ambayo amebaini katika rufani hiyo ni kuwasilishwa bila kuwekwa mhuri hati ya kukaza hukumu (tuzo) iliyotolewa na Jaji aliyetoa hukumu katika kesi ya awali. “Hapa nani ambaye anajua sahihi ya Jaji? Alihoji. Hawa mawakili walipaswa kushinikiza kuwekwa mhuri wa mahakama katika hukumu hiyo ili kuthibitisha uhalali wake,” alisema Alute. Hata hiyo, wakili huyo alisema badala yake, mawakili hao waliwasilisha mahakamani rufani hiyo ndani ya siku 29 tu baada ya hukumu, badala ya siku 60 ambazo walipewa.

 “Kwa kuwasilisha mahakama ya rufani, hukumu ambayo bado haina mhuri wa Jaji ni ukiukwaji wa kanuni na taratibu za mahakama.” Mughwai alidai kuwa katika mazingira ya sasa hakuna cha kurekebishwa katika rufani hiyo, badala yake itupwe na kuwataka wakata rufani kulipa gharama zote za kesi. Hata hivyo, hoja hizo zilipingwa na mawakili wa Lema ambao ni Tundu Lissu na Method Kimomogoro, ambao walidai kuwa hawakuwa na mamlaka ya kumlazimisha Jaji Rwakibarila kuweka mhuri. 

Lissu alidai "Kama inaonekana sasa kuwa ni batili, basi hata uamuzi wa kumvua ubunge Lema ni batili," alisema. Wakili Kimomogoro Kwa upande wake, Wakili Kimomogoro alisema kisheria kasoro hizo ya mhuri wa mahakama na tarehe, haziwezi kusababisha rufani hiyo kutupwa kwani haziathiri madai ya msingi katika rufani. 

Alidai kesi hiyo ya Lema ilikuwa ya kipekee kwani mara tu baada ya hukumu kutolewa faili lilipelekwa jijini Dar es Salaam na maombi ya nyaraka kadhaa za kesi hiyo yalitumwa kutoka Dar es Salaam. “Katika mazingira kama haya hatuwezi kuepuka makosa ya kibinadamu ambayo yanatambulika kisheria,” alidai Kimomogoro. Aliongeza kuwa katika hoja hiyo, waliandika kifugu namba 114 badala ya 113 kimakosa ya kiuchapaji, lakini hakipotoshi kitu chochote kwani kifungu hicho hakipo. Wakili Kimomogoro alisema wakili mwenzake, Mughwai ameshindwa kuzungumzia uamuzi ya kesi ambazo, hazikufutwa kutokana na kuwa na upungufu mdogo wa aina hiyo ambao kimsingi hauathiri rufani. 

Hata hivyo, alisema kama wakili huyo alibaini makosa hayo, katika uwasilishaji wa hoja zake, alipaswa pia kurekebisha kwa mujibu wa sheria ya mwaka 2009 ya mahakama. Kimomogoro pia aliwasilisha mahakamani hoja kadhaa za kisheria na uamuzi ya Mahakama ya Rufani za ndani na nje ya nchi, ambazo hazikutupilia mbali rufani ambazo zilikuwa na upungufu mdogo, kwani lengo la mahakama hizo ni kutafuta haki.

 “Siyo kila kasoro au usumbufu kwenye hukumu unaweza kusababisha kutupwa rufani kwani kasoro zote zilizotajwa ni za makosa na uchapaji na nyingine ni za kiutaratibu tu,” alisema. Alifafanua kuwa makosa ambayo yanaweza kusababisha rufani kutupwa ni kama aina namba ya kesi, majina na wadhifa wa wadau katika shauri husika, mambo yanayolalamikiwa na mahakama imeamua nini. 

Wakili huyo alifafanua kuwa jambo la kukosekana mhuri wa mahakama wa Jaji siyo kubwa na kusababisha kutupwa rufani kwani hakuna ambaye anapinga hukumu iliyowasilishwa mahakamani. Kwa upande wake, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Vitalis Timoth alisema anaunga mkono hoja za mawakili wa Lema, kuwa pingamizi ya wakili Mughwai haina msingi wa kisheria. 

Alisema hati ya kukaza hukumu (Tuzo) inatolewa chini ya sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai na siyo chini ya sheria ya masijala za mahakama. Alisema siyo kazi ya jaji aliyetoa hukumu, kuweka mhuri hukumu yake bali hiyo ni kazi ya msajili wa mahakama na masijala za mahakama.

 “Kama hati ya kukaza hukumu ina matatizo anayepaswa kulaumiwa siyo mawakili bali ni mahakama ambayo ndiyo ilikuwa na mamlaka ya kuweka mhuri,” alisema. Alidai kuwa pingamizi ya awali ya rufani inapaswa kuwa na sifa mbili, kwanza iwe na suala la kisheria na pili iendane na kesi ya msingi. “Katika hoja za wakili Mughwai ni wazi inathibitika pingamizi hili halina matakwa ya kisheria kwani hata kama ikipitwa siyo kuwa itazuia kurejeshwa tena na kusikilizwa kwa rufani ya msingi.” Alidai ni busara kuacha kuwa na pingamizi ambazo zinaongeza gharama za kesi na muda wa kusikiliza.

 “Ushauri wangu kila shauri liamuliwe kwa mazingira yake na uamuzi wa sasa uzingatie mahakama katika kutenda haki,” aliongeza. Alidai kwamba kutupwa kwa hoja ya kutaka waomba rufani wachapwe mijeledi kwani kazi ya mahakama siyo kuchapa watu bali ni kutoa haki. “Tunashauri kusikilizwa rufani kwa kuzingatia sheria na ushahidi,” alisema. Jopo la Majaji Baada ya kutolewa kwa hoja za pande zote za mawakili, Jaji Chande na Jaji Massati waliwauliza maswali kadhaa mawakili hao na kujieleza na baadaye Jaji Chande alitangaza kuahirishwa kwa kesi hiyo hadi hapo itakapotangazwa. Jaji Chande alisema vikao vya Mahakama ya Rufani Kanda ya Arusha vimemalizika jana, hivyo uamuzi wa kutupwa kwa pingamizi la rufani hiyo au la utatolewa siku itakayopangwa na mahakama.

 Baada ya uamuzi huo umati wa wafuasi wa Chadema, uliokuwa ndani na nje ya mahakama ulianza kuimba nyimbo mbalimbali kama vile Lema Jembe na bila Lema patachimbika. Katika hatua ya kuepuka vurugu, Lema alizungumza na wafuasi hao nje ya mahakama na kuwataka kuondoka kwa amani kwenda katika ofisi ya Chadema iliyopo Ngarenaro kwa amani bila vurugu. 

Warufaniwa katika kesi hiyo ni makada wa CCM, Happy Kivuyo, Mussa Mkanga na Agnes Mollel ambao walishinda kesi ambayo hukumu yake ilimvua ubunge Lema Aprili 4, mwaka huu.
Chanzo:Mwananchi.co.tz

Wednesday, 5 September 2012

TENDWA KUIFUTA CHADEMA

Msajili wa vyama vya siasa nchini John Tendwa amesema sasa amechoka kusikia mauaji kwenye mikutano ya kisiasa ya CDM na atatumia rungu lake kufutia usajili chama chochote kitakachoshindwa kutunza amani ya nchi.Tendwa amewaambia waandishi wa habari hatishiki na chama chochote kuwa na wabunge kwani sheria inamruhusu kufuta chama hata kama kina wabunge 100.

Katika hali ya kushangaza Tendwa ameshauri vyama visubiri nyakati za uchaguzi ndipo vifanye mikutano ya kisiasa.Hata hivyo amekiri sheria inaruhusu vyama kufanya mikutano na maandamano wakati wowote.

Source:Habari Radio Tumaini.

MAGAZETI YETU YA LEO








Chanzo,www.mjengwablog.com

Friday, 31 August 2012

GAVANA AZINDUA MFUKO WA KUNUNUA DHAMANA

GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndullu akiongea na waandishi wa habari  jijini Dar es salaam kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo mfumo wa mawakala wa Benki hiyo wa kununua dhamana za Serikali na hati fungani kwa njia ya mtandano(online) kwenye mnada na hivyo kupunguza ule utaratibu wa dhamana wa kupeleka karatasi katika Benki ili kupata huduma hiyo.

Monday, 27 August 2012

UJUMBE WA KIPANYA LEO


HUU HAPA MSIMAMO WA MNYIKA JUU YA VURUGU ZILIZOTOKEA MOROGORO

Niliwahi kutahadharisha baada ya tukio la Dkt Stephen Ulimboka kuwa serikali imeanza kutumia mbinu haramu kudhibiti fikra mbadala, CCM imeanza kuongoza serikali kiimla na ipo siku umma utafikia hatua ya kukiona kama chama cha mauaji. Raia watatu wasio na hatia wamefyatuliwa risasi na mmoja amefariki. Haya yamefanyika kwenye maandamano ya amani ya wananchi kuwapokea viongozi wa CHADEMA kuelekea kwenye mkutano. Vurugu zimeanzishwa na polisi kwa mujibu wa mashuhuda wa ushahidi wa video. Vyanzo vyangu vinaniambia sasa wameagiza gari tatu za FFU na gari za kuwasha toka Dar Es Salaam. Tuombe MUNGU wasiamue kuvuruga mkutano wa hadhara ambao wananchi wamekusanyika kwa wingi hivi sasa. States captured by grand corruption of the ruling party cronies for so many years resorts to bullets as a way of stopping M4C through the ballot. Maisha ya wachache yako mashakani lakini si mabadiliko kwa maslahi ya wengi.

John John MNYIKA,
27 Agosti, 2012

WAKULIMA WA MPUNGA KATAVI WANUSURIWA

 
Waziri MKUU Mizengo Pinda
Magreth Munisi
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewataka wakulima wa mpunga nchini kuanza kujipanga kuuza mchele nje ya nchi.
Pinda alisema hayo juzi wakati akikagua kazi ya kuweka mitambo ya kinu cha kukoboa mpunga katika kata ya Mwamapuli na Majimoto wilayani Mlele mkoani Katavi, na ujenzi wa madaraja ya mto Msadya na mto Kavuo.

Aliendelea kusema kuwa kulingana na mahitaji yatakayokuwepo, wakulima hao kama watajipanga vizuri wanaweza kuuza mchele watakaouzalisha hadi katika nchi za Burundi na Rwanda ambako soko la uhakika lipo.

“Kwa mahitaji yatakayokuwepo, na kama wakulima watajipanga vizuri wanaweza kuuza mchele mpaka nchi za Rwanda na Burundi,” alisema Pinda kwenye taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na ofisi yake.

Aliendelea kufafanua kuwa kukamilika kwa mradi huo kutawasaidia wakulima kuuza mchele badala ya kuuza mpunga, ndipo alipoelekea Mwampuli kukagua kinu hicho kilichonunuliwa kwa fedha za Halimashauri kwa lengo la kuwasaidia wananchi wa kata hizo

Kwa upande mwingine, diwani wa kata hiyo, Emmanuel Mponda alimweleza Waziri Mkuu kuwa kinu hicho kina uwezo wa kukuboa tani 300 kwa siku kikiendeshwa kwa saa nane kutwa nzima.

Diwani huyo alieleza kuwa kinu hicho kina uwezo wa kuchambua mchele na kuupanga katika madaraja manne tofauti na kuufungasha kwa madaraja hayo, na kinatarajiwa kuanza kazi Septemba mara jenereta litakapokamlika kuunganishwa.
“Mchele ukishakobolewa, unapangwa katika madaraja A, B, C, na daraja D zinakuwa ni chenga ambazo zitauzwa peke yake kwa ajili ya wauza vitumbua. Kinu hiki pia kina uwezo wa kutenganisha pumba kwa ajili ya mifugo na kuzipaki katika sehemu ya peke yake bila kuingiliana na uzalishaji wa mchele,” alisema Mponda.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda Vijijini, Wilbroad Mayala alisema kinu hicho kimegharimu Sh96 milioni wakati jenereta la kuendesha kinu hicho lenye uwezo wa kuzalisha kilowati 120, limenunuliwa kwa sh86 milioni.
Chanzo:mwananchi.co.tz

HII NI TASWIRA YA NAMNA WATU WALIVYOJITOKEZA KATIKA MKUTANO WA M4C MOROGORO

PICHA MBILI ZA KIJANA ANAEDAIWA KUUWAWA NA POLISI HUKO MOROGORO KATIKA MAANDAMANO YA CHADEMA





Hizi ni baadhi ya picha za kijana anaedaiwa kuuwawa katika maandamano ya CHADEMA huko Morogoro.

NAPE AKATAA KUIOMBA RADHI CHADEMA



Akataa kuomba radhi, asema tuhuma atazithibitisha mahakamani, Amtaka Dk. Slaa kuandaa bilioni 3 na shilingi moja. Ni kwa kudai CCM inaingiza silaha nchini.

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa Itikadi na Uenezi CCM, Nape Nnauye amewataka Chadema kwenda mahakamani haraka badala ya kusubiri kuombwa radhi kama walivyotaka ili kusafishwa dhidi ya madai ya chama chao kupewa mabilioni ya fedha na mataifa tajiri.

Aidha amemtaka Katibu Mkuu wa chama hicho Dk. Wilbrod Slaa kuiomba radhi CCM la sivyo itamburuza mahakamani kudai fidia ya sh. bilioni 3 na shilingi moja, kwa kuituhumu uongo kwamba imeingiza silaha kutoka nje ya nchi tena bila kulipia ushuru.

Nape alisema hayo leo Agosti 27, 2012, kwenye mkutano wake na waandishi wa habari, uliofanyika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, mtaa wa Lumumba mjini Dar es Salaam.

"Bila shaka mmesikia jana Chadema wakinitaka niombe radhi au wananipeleka mahakamani kudai fidia ya sh. bilioni 3, kwa madai eti nimesema Chama hicho kinapata mabilioni ya fedha kutoka kwa mataifa tajiri. Mkubwa hatishiwi nyau, nawataka waende haraka mahakamani wala wasisubiri hizo siku saba", alisema Nape.

Alisema, CCM inao ushahidi wa kutosha kuhusu madai aliyotoa Nape dhidi ya Chadema na kwamba huyo tayari kutoa uthibitisho huo mahakamani badala ya kuomba radhi.

"Nadhani wakienda mahakani itapendeza zaidi maana huko ndiko pazuri kutoa uthibitisho kuhusu tuliyosema, na ninawahakikishieni tukishathibitisha na Msajili wa Vyama akaupata uthibitisho huo chama chao kinafutwa", alisema.

Kuhusu CCM kumburuza Dk. Slaa mahakamani, Nape alisema, ameshawaagiza wanasheria wa Chama, kuandaa barua ya kusudio la mashitaka hayo, na Dk. Slaa atapelekewa ili aamue kama ataomba radhi au atakuwa tayari kwenda mahakamani.

"Wakati wanakwenda mahakamani, Chadema wamwambie babu yao ajiandae kuomba radhi au kuburuzwa mahakamani kuilipa CCM fidia ya sh. bilioni 3 na shilingi moja kwa kuizushia CCM uongo kwamba inaingiza silaha nchini tena", alisema Nape.

Bashir Nkoromo
Blogger & Senior Photojournalist
Uhuru Publications Ltd,
Publishers of Uhuru, Mzalendo and Burudani tabloids
Cell; +255 712 498008, +255 789 498008, +255 773 600007 +255 756 646131
E-mail: nkoromo@gmail.com, bnkoromo@yahoo.com. 
P O Box 9221, Dar es Salaam.Tanzania, East Africa