search

.

Wednesday, 11 July 2012

MGOMBEA UMAKAMU MWENYEKITI YANGA AZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI, AMWAGA SERA ZAKENDUGU zangu wanahabari, nimewaiteni leo kuzungumza nanyi kama mnavyofahamu nawania nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Yanga.


Nimejitosa kuwania nafasi hii nikiamini nina uwezo na sababu ya kuiongoza Yanga, ili niweze kutoa mchango wangu kwa klabu ninayoipenda tangu utotoni.


Ili ndoto za yale ninayofikiri ni muhimu katika vipaumbele vyangu, kwa kushirikiana na viongozi wenzangu sanjari na wanachama, kwanza kabisa kutengeneza mfumo ambao mipango yake inatekelezeka.


Mfumo huo wa awamu tatu tofauti, tukianzia mipango ya muda mfupi, muda wa kati na mipango ya muda mrefu, ambao hata kama muda wetu wa kukaa madarakani utamalizika, itawawia rahisi viongozi wajao kuongoza kwa kufuata mfumo zaidi ambao utarahisiha utekelezaji wa majukumu yao.


Kama nikipata ridhaa ya kuiongoza Yanga kuna mambo ambayo nitayapa kipaumbele ikiwemo suala la marekebisho ya Katiba.


Kwa kushirikiana na viongozi wenzangu, lakini kwa kuwashirikisha zaidi wanachama tutaipitia upya Katiba na kuifanyia marekebisho, ili tuwe na Katiba imara, yenye nguvu itakayoletea tija.


Kwa sasa Yanga haina dira wala mwelekeo. Tunahitaji kuwa na dira na mwelekeo, bila hivyo hatutafika popote, hivyo nikiingia madarakani kwa kushirikiana na viongozi wenzangu mtazamo wangu utakuwa katika kujenga mfumo wa kudumu katika masuala yafuatayo.


(1)              Umoja: Kusimamia suala la umoja na mshikamano ndani ya klabu na kuondoa makundi na kuhakikisha Yanga inakuwa moja kwani haiwezekani mwana- Yanga adui yake, awe mwana Yanga, hivyo umefika wakati mambo hayo yaondolewe.


Ili kuimarisha uhusiano na kujenga umoja ndani ya Yanga, tutahakikisha vikundi vyote vilivyomo ndani ya klabu vinatambuliwa kikatiba ili viweze kuendelea kuisaidia klabu kwa utaratibu ulio rasmi.


Hii nikimaanisha viongozi wa matawi Tanzania nzima, Wazee, vijana na hata vikundi vya ushangiliaji vinavyoleta hamasa katika michezo yetu mbalimbali.
(2)              Soka la vijana: Nitahakikisha natilia mkazo kuendeleza soka la vijana na kuibua vipaji vipya kama ilivyokuwa miaka ya zamani.


Mpira si kama paa la nyumba kwamba siku zote linakuwa juu tu, soka inaanza chini hivyo ni vyema watu wakatambua hilo, ili mchezo huu upige hatua kama zilivyo nchi zilizoendelea duniani, ni lazima utengenezwe msingi kwanza kwa kuchagua vijana wadogo, ambao baadaye watakuwa hazina kwa Yanga.


(3)              SACCOS- Kuwafanya wana Yanga wajivunie zaidi klabu yao, tutapanua wigo wa taasisi yetu, kwa kuanzisha Mfuko wa Akiba na Mikopo kwa wanachama (SACCOS), ambao utakuwa ukitoa mikopo kwa wanachama wake, kupitia matawi jambo ambalo litaondoa utegemezi katika klabu na hata miongoni mwa wanachama.


(4)              KUJITEGEMEA: Tutabadili mfumo wa uendeshaji klabu uendane na hali ilivyo ya soka la sasa, ambapo klabu inatakiwa kujiendesha kibiashara, kwani Yanga ni taasisi kubwa yenye fedha nyingi, ambazo zikitumika ipasavyo, zitaisaidia timu kiuchumi na kujiendesha kisasa na jambo hilo litawezekana iwapo tutakuwa na Katiba bora ambayo itawezesha jambo hilo kutekelezeka kiurahisi.


Ni aibu klabu kubwa kama Yanga kuwa maskini, wakati ina raslimali za kutosha ambazo haziinufaishi, hivyo kubadili mfumo wa uendeshaji kutaifanya iweze kujiendesha kwa kujitegemea.


Nia sio kurudi nyuma bali kwenda mbele na kuondoa umaskini uliokithiri katika klabu yetu na kuifanya ijiendeshe kisasa na kuwa klabu ya kulipwa ambayo inaweza kukabiliana na klabu nyingi kubwa za Afrika.


Kwa kushirikiana na viongozi wenzangu nitaweka mawazo ya kuifanya Yanga iweze kujiendesha kibiashara na ikiwezekana kubadili katiba kwa kutilia mkazo suala la kampuni ili tuweze kuuza hisa za klabu, jambo ambalo litasaidia kuongeza mapato pamoja na kuwajibika kwa wanachama ambao sasa watakuwa sehemu ya klabu kwa karibu zaidi.


(5)              UENDESHAJI WA KLABU: Pia katika kuboresha mfumo huu wa uendeshaji, tutaunda idara kadhaa kwa ajili ya kurahisisha suala hilo, ambapo kutakuwa na Idara za Uhasibu, Masoko, Sheria pamoja na ile ya Habari, Mawasiliano na Uhusiano.
Pia shughuli zote zinazohusu klabu zitafanyika makao makuu ya klabu yetu Jangwani, hivyo mawasiliano yoyote ya kikazi baina ya wachezaji, viongozi, wanachama na wadau wa Yanga yatafanyika klabuni lengo ni kuongeza heshima na uadilifu kwa Yanga.


Ili kulipa nguvu suala hilo tutalifanyia ukarabati jengo la makao makuu ya klabu liwe na hadhi ya Yanga na kwa ujumla uongozi wangu kwa kushirikiana na wenzangu utakuwa ule unaozingatia zaidi Katiba.


(6)              MATAWI: Nitahahakikisha uongozi wangu unaimarisha matawi ya klabu na kufanya wanachama kufahamu na kuchangia shughuli za klabu na kwa kuanzia itakuwa busara kila wilaya zilizopo jijini Dar es Salaam kuwa na ofisi na vitendea kazi muhimu na mpango huo utaendelea nchi nzima.


Lakini pia lazima niwe muwazi tangu sasa, kuwa si kila jambo litahusisha wanachama wote,  mfano mipango ya timu kwa maana ya usajili, ushiriki wa ligi na michuano ya Kimataifa, hilo likishikwa na watu wengi nafasi yake ya mafanikio huwa ndogo, tutazipa nguvu kamati za ufundi na mashindano kufanya kazi kwa wepesi na ushirikiano mkubwa.
KAULI YANGU KWA WANA-YANGA:


Naomba wanichague mimi wajenge imani kwangu kwani nitahakikisha kwa kushirikiana na wenzangu tunajenga timu imara ya ushindani, itakayokuwa tishio katika michuano ya ndani na ya kimataifa. Wamchague Sanga kwa Yanga inayoeleweka.


SANGA KWA YANGA INAYOELEWEKA.