search

.

Thursday, 18 October 2012

MWANAMKE MSHIRIKINA AONYESHA NGOZI YA MTOTO WA MIAKA MIWILI

Mwanamke aliyejitambulisha kwa jina la Belikumana Lugome(48), Mkazi wa Kijiji cha Parangu Songea Mkoani Ruvuma amekiri kujihusisha na imani za kishirikina na kukabidhi sehemu ya madawa aliyokuwa akiyatumia kwa Mganga wa Jadi aliyefahamika kwa jina la Jesca Ndembo Mkazi wa Iyunga Mkoani Mbeya.

Mwanamke huyo alifika kwa Mganga huyo wa jadi Oktoba 12 mwaka huu, majira ya saa 8 mchana alipokwenda hapo kwa nia ya kumwangalia shangazi yake aliyekuwa akitibiwa na Mganga huyo.

Aidha imedaiwa kuwa shangazi yake huyo alirogwa na nduguye na mshirikina huyo kukiri kwamba ndiye alisababisha upasuaji wa tumbo lake mara mbili na kutakiwa apasuliwe tena na kama asingewahi angeuawa kwa siku za hivi karibuni.

Bi. Lugome amekiri kujihusisha na matukio ya ajali 15 mkoani Ruvuma na kusababisha vifo vya watu 15 katika ajali hizo.

Aidha alionesha sehemu ya vifaa ambavyo alikuwa akivitumia katika ushirikina ikiwemo ngozi ya mtoto wa miaka miwili.

Hata hivyo amesema kuwa yeye aliupata uchawi huo kutoka kwa Waganga mbalimbali Mkoani Ruvuma na kwamba hapendi hali hiyo kwani haina faida yoyote. 

CHAMI AIBUKA KIDEDEA CCM-NEC MOSHI VIJIJINI


Mbunge wa Moshi vijijini Dr. Cyril August Chami ameibuka kidedea katika uchaguzu wa mjumbe wa nec kupitia wilaya ya moshi vijijini. Dr. Chami alipata kura 967 (96%) kati ya kura 1008 zilizopigwa. katika uchaguzi huo ndugu Gabriel masenga alitetea nafasi yake ya mwenyekiti wa ccm
wa wilaya ya moshi vijijini.

MH MNYIKA NA MUSWADA KWA HATI YA DHARURA

Mwanzoni mwa wiki tarehe 15 Oktoba 2012 niliwasilisha kwa Katibu wa Bunge kusudio la kuwasilisha Muswada Binafsi wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Sheria za Hifadhi ya Jamii (The Social Security Laws (Ammendments) Act wa mwaka 2012 kwa hati ya dharura kwa mujibu wa Kanuni ya 81 ya Kanuni za Kudumu za Bunge (Toleo la Mwaka 2007) iwapo Serikali haitatoa kauli kwa umma ya ratiba ya kupata mapendekezo toka kwa wadau wa hifadhi ya jamii pamoja na kamati husika ya kudumu ya Bunge kwa kuzingatia kuwa vikao vya kamati za kudumu za bunge vimeanza tarehe 15 Oktoba 2012 bila suala hilo kuzingatiwa.

Nimefikia uamuzi huo kwa kuwa mpaka sasa ikiwa zimebaki siku chache Mkutano wa Tisa wa Bunge kuanza tarehe 30 Oktoba 2012 ambao Serikali iliahidi kuwa italeta marekebisho ya Sheria ya Hifadhi ya Jamii, mpaka sasa Serikali haijaitisha mkutano na wafanyakazi pamoja na wadau wa jamii kupokea mapendekezo hali ambayo inaashiria upo uwezekano muswada huo usiwasilishwe kwa wakati.

Lengo la Muswada huo ni kufanya marekebisho yenye kuboresha mfumo wa utoaji wa mafao nchini ikiwemo kuwezesha kutolewa kwa fao la kujitoa (withdrawal benefits) na mafao mengine muhimu ambayo hayatolewi katika utaratibu wa sasa wa mifuko mbalimbali ya hifadhi ya jamii.

Kwa upande mwingine kufutwa kwa mafao ya kujitoa msingi wake haupo kwenye marekebisho ya sheria yaliyofanyika tarehe 13 Aprili 2012 pekee bali ni udhaifu katika mfumo mzima wa kisera na kisheria wa hifadhi ya jamii nchini hali ambayo inahitaji wadau kutaka mabadiliko makubwa.

Hivyo, Waziri wa Kazi na Ajira kutoa kauli kwa umma kuhusu maelekezo aliyoyatoa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) baada ya mkutano wa nane wa Bunge kufuatia mapendekezo niliyotoa bungeni ya kuitaka Wizara husika kutoa muongozo wa kisera wa kutengua taarifa kwa umma iliyotolewa ya kueleza kuwa “kufuatia kuanza kutumika kwa Sheria hiyo (ya 13 Aprili 2012) maombi mapya ya kujitoa yamesitishwa kwa kipindi cha miezi sita hadi pale miongozo itakapotolewa ili kuwezesha Mamlaka na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kutoa elimu kwa Wadau”.

Wenu katika uwakilishi wa wananchi:
John Mnyika (Mb)

SHAMBULIO LA GURUNETI LAUA WATATU MOMBASA

 Maafisa wa polisi wa Kenya wakilinda nyumba katika kitongoji cha Likoni mjini Mombasa baada ya uvamizi wa polisi tarehe 17 Oktoba. [Na Stringer/AFP]
Maafisa tisa wa polisi walijeruhiwa katika shambulio la guruneti wakati wa uvamizi dhidi ya ugaidi katika eneo  la Mombasa  Kenya.
Watuhumiwa wawili wa ugaidi waliuliwa wakati wa uvamizi huo, na mmoja wa maafisa wa polisi waliojeruhiwa alifariki baadaye kutokana na majeraha akiwa hospitali.
 Police kutoka Kitengo cha Kupambana na Ugaidi walikuwa wanajaribu kuwakamata watuhumiwa wa ugaidi wakati wafuasi wa al-Shabaab walipowarushia guruneti, alisema Mkuu wa Polisi wa Mkoa wa Pwani Aggrey Adoli.
Alisema kuwa kabla ya hapo polisi walikuwa wamemtia mbaroni mshukiwa moja huko Changamwe ambaye aliwaongoza hadi kwenye nyumba.
"Tulipofika nyumbani hapo, wale waliokuwemo ndani walikataa kufungua na badala yake [mmoja wao], aliwarushia guruneti maafisa, na kumuua mwenzao na kuwajeruhi maofisa wetu. Baadaye aliuliwa wakati wa kutupiana risasi," Adoli alisema.
Polisi walipata bastola moja, bunduki aina ya AK-47, maguruneti mawili na risasi 15, kwa mujibu wa Adoli. Aliongeza kuwa ukamataji zaidi utafanywa pale askari watakapofanya juhudi za kupambana na ugaidi.

PICHA MBALI MBALI ZA MAZISHI YA MAREHEMU KAMANDA LIBERATUS BARLOW
 Mafundi wakiwa katika harakati ujenzi wa nyumba ya milele (Kaburi) ya Aliekuwa Kamanda wa Polisi Mkoani Mwanza,Marehemu Liberatus Barlow (RPC) huko kijijini kwao Kilema Kioo,Mkoani Kilimanjaro mapema leo asubuhi.Marehemu Liberatus Barlow (RPC) aliuwawa kwa kupigwa risasi na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi huko Kitangiri,jijini Mwanza hivi karibuni.
Hii ni sehemu iliyotengwa maalum kwa viongozi.
 Viongozi mbali mbali wakiwa kwenye Misa ya Kuuaga Mwili wa Marehemu.
 Mwili wa Marehemu ukiwasili Nyumbani.
 Brass Band ya Polisi ikiongoza 

 Misa ikiendelea

Wednesday, 17 October 2012

MAGGID MJENGWA: MBAGALA NA BEDUI ALIYEKOJOA MSIKITININdugu zangu, 

 Moja ya hadithi za Mtume Muhammad S.A. W ni pale Mtume Muhammad alipokuwa msikitini na maswahaba wake. Mara akaingia msikitini mtu wa kabila la Mabedui na kuanza kukojoa. Maswahaba wa Mtume wakasimama kwa hamaki kutaka kumwadhibu Bedui yule. 

Mtume akawasihi maswahaba wake wasifanye jambo lolote litakalomdhuru Bedui yule. Hapo ikavutwa subira. Bedui yule akakojoa na akamaliza. Mtume Muhammad alipomuhoji Bedui yule ikabainika kuwa alikuwa ni mtu wa hovyo na wala hakujua kuwa alimokuwa ni msikitini. Bedui yule akaelimishwa, akaelewa. Akarudi kwenye ustaarabu. 

Ndio mkojo ule ulifutwa kwa maji na amani ikawepo. Wahenga walinena; Subira yavuta heri. Siku zote, hamaki si jambo jema. Kwa kutanguliza subira na kutumia hekima Mtume Muhammad aliivuta heri na kuepusha shari. 

Maana, kama Mtume alisingewaasa maswahaba wake kuvuta subira, basi, makubwa matatu yangetokea ndani ya msikiti ule; Mosi, zingezuka vurugu na watu kuumizana na hata kutoana roho. Pili, mkojo wa Bedui yule ungesambaa msikitini kwa vile alishaanza kukojoa na isingekuwa rahisi kwake kukatisha mkojo wake. Tatu, Mkojo una madhara ya kiafya pia. 

 Naam, kwa mwanadamu, ni muhimu kuwa na subra na kutafakari kabla ya kufanya maamuzi. Kwa ndugu zangu Waislamu, tunaona Mtume Muhammad ameweza kuonyesha hilo. Na kwa ndugu zangu Wakristo, kuna mifano pia ya Yesu Kristo kuonyesha subra. 

Ndio, Uislamu, kama ilivyo kwa Ukristo na dini nyingi za humu duniani, msingi wake ni amani na upendo. Kitendo cha mtoto yule wa Mbagala kukojolea korani kitazamwe kwa sura ya kitendo kilichofanywa na mtoto . 

Na kama ilivyokuwa kwa Bedui yule, kama pale Mbagala subira na hekima vingetangulizwa, basi, yumkini tungebaini kuwa mtoto yule hakujua madhara ya kitendo chake. Naye angekanywa kama tuwakanyavyo watoto wetu. Na hata kitendo hicho kingefanywa na mtu mzima, bado tulikuwa na haja ya kutanguliza subira na hekima kumhoji aliyetenda, yaweza akawa kama Bedui yule kwenye msikiti alimosali Mtume na maswahaba wake. 

Na kwa kuangalia picha zile za Mbagala naiona hatari iliyopo sasa, kuwa tuna vijana wengi wasio na kazi; Wakristo kwa Waislamu. Vijana wasio na dogo. Ni kama moto uliofifia. Akipatikana kwa kuchochea kuni wanalipuka. 

Ni vijana wanaopatikana wakati wowote na mahali popote. Hata jambo likianza saa tatu asubuhi wao wapo. Hawana ofisi wala bosi wa kumwomba ruhusa ya kwenda kuandamana na kurusha mawe. Ndio hawa wanaonekana wamevaa ' Kata kiuno' na wengi wao hawajahi hata kuingia misikitini au makanisani. 

Inakuawaje kijana wa kweli wa Kiislamu achome kanisa na kuiba kompyuta. Inakuawaje kijana na muumini wa kweli wa Kiislamu aonekane saa mchana wa jua kali akivamia baa na kukimbia na kreti za bia? Ni maswali yanayotutaka tutafakari kwa makini. 

Maana, ninavyoamini mimi, uchumi na elimu duni ndio hasa vinavyochochea  vurugu za kijamii, iwe za kidini au kisiasa, na hususan inapohusisha vijana.   Vijana wetu hawana misingi mizuri ya elimu, na wengi hawana ajira pia. Haya ni sawa na makombora yasiyo na gharama kubwa kuweza kutumiwa na wanasiasa wasio waadilifu na hata viongozi wa kidini wenye mitazamo mikali.  Ni makombora yaliyoanza kutulipukia. Tuliziona ishara, tukazipuuzia. 

Leo  Kuna vijana watakaotumiwa au kutumia fursa hiyo kutenda maovu kwa kisingizio cha dini. Ni hawa wataoshiriki kuchafua taswira za dini husika pia. Tujiadhari, kabla ya hatari kubwa inayotujia. Hatujachelewa.

 Na hilo ni Neno La Leo. 

Maggid Mjengwa, 

Iringa. 

0788 111 765
Chanzo:www.mjengwablogspot.com

KURASA ZA MBELE ZA MAGAZETI YETU LEO ALHAMISI 18 OCTOBER 2012


Chanzo.www.Mjengwa.blogspot.com

PICHA MBALI MBALI ZA VURUGU ZA ZANZIBARvurugu mtaani

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU VURUGU ZILIZOTOKEA ZANZIBAR
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imewataka wananchi kuendelea na shughuli zao kama kawaida na kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vimedhibiti hali ya ulinzi na imeimarishwa katika maeneo yote ya Zanzibar.

 Taarifa ya Serikali iliyotolewa leo usiku na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed imesema Zanzibar bado ni shwari na inaendelea kuwa katika hali ya amani na utulivu. Akizungumzia tukio la vurugu zilizofanywa na wananchi wachache, Waziri Mohamed Aboud alisema vikundi vya vijana vinavyosadikiwa kuwa ni wafuasi wa Sheikh Farid Hadi walifanya vurugu hizo katika mitaa ya Darajani, Michenzani, Muembeladu,Magomeni,Amani wakidai Sheikh wao haonekani na kudhani amekamatwa na vyombo vya Dolan a kuwekwa ndani. 

Waziri Mohamed Abud alisema Serikali imewasiliana na vyombo vya Dola ikiwemo Polisi,Jeshi la wananchi wa Tanzania, Idara ya Usalama wa Taifa, Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,KMKM,JKU,Chuo cha Mafunzo,Zimamoto na Valantia ambapo vyombo vyote hivyo vimeeleza kutoelewa chochote kuhusu Sheikh Farid. 

Waziri huyo alisema kwamba Jeshi la Polisi limepokea taarifa ya kutoonekana kwa Sheikh Farid ambapo kwa sasa Jeshi hilo linaendelea kumtafuta na kufanya uchunguzi juu ya tukio hilo ili kupata ukweli wake na kuchukua hatua zinazofaa. Alisema kwamba wakati Jeshi la Polisi likiendelea na upelelezi wake, wananchi wameombwa kutoa taarifa kuhusu tukio hilo kwa vituo vya Polisi au kupitia Masheha, Ofisi za Wilaya na Mikoa katika maeneo yao.

 Waziri Mohamed Aboud amesema Serikali inawasihi wwananchi waache kujiingiza katika vitendo vya fujo na vurugu kwani kutenda hivyo ni kosa kwa mujibu wa sheria na Serikali haitovumilia vitendo hivyo. Katika tukio la leo mchana, vijana hao wanaosadikiwa kuwa ni wafuasi wa Sheikh Farid Hadi walifanya vitendo vya vurugu ikiwemo kuchoma moto Maskazini za CCM,kuvunja maduka,kupora mali za watu na kuharibu miundombinu ya barabara na kusababisha hasara kubwa.

 IMETOLEWA NA: IDARA YA HABARI(MAELEZO) ZANZIBAR 17/10/2012 ZANZIBAR,TANZANIA

PONDA AKAMATWA, WAUMINI WAANDAMANA

KATIBU wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Issa Ponda amekamatwa na Jeshi la Polisi usiku wa kuamkia leo jijini Dar es Salaam. Sheikh Ponda amekamatwa pamoja na wenzake wapatao 49 wakiwemo wanawake 12, wanaume 37 kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo uchochezi dhidi ya Serikali. Kufuatia tukio hilo, baadhi ya waislamu mchana huu wameandamana kwenda kituo cha Polisi Kati kwa ajili ya kushinikiza kuachiwa kwa Sheikh Ponda na waislamu wenzake. Waandamanaji hao walitawanywa na polisi wakati wakijaribu kuingia kituoni hapo.

ZAMBI ATWAA UENYEKITI WA CCM MBEYA


Mbunge wa Jimbo la Mbozi Mashariki Godfrey Zambi ameshinda nafasi ya Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mbeya.
Zambi kapata kura 888  na kufuatiwa na Allan Mwaigaga ambaye amepata kura 318 na kufuatiwa na Reginald Msomba aliyepata kura 237


Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima ndiye alikuwa msimazi wa uchaguzi huu akitangaza matokeo


Mwenyekiti  wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mstaafu mkoa wa Mbeya, Nawab Mullah, akimkaribisha mwenyekiti mpya Mh Zambi

Allan Mwaigaga ambaye amepata kura 318 na kuwa mshidi wa pili akiwashukuru wanachama wa ccm katika uchaguzi huo na kusema sasa makudi yavunjwe maadam mshindi kapatikana 


Reginald Msomba aliyepata kura 237. mshindi wa tatu nae pia akiwashukuru wanachama wa ccm katika uwanja wa sokoine jijini mbeya

Mkuu wa mkoa Mbeya Abasi Kandoro kulia katikati  chales Mwakipesile kushoto kabisa mwenyekiti mstaafu mulla wakiwa makini kufuatilia matokeo uwanjani hapo  mida ya saa sita kamili usiku

wanachama wa ccm wakiwa makini kusikiliza matokeo uwanjani hapoMwenyekiti mpya Zambi akipongezwa na mwenyekiti mstaafu Mullah mara baada ya kutangazwa mshindi

Baadhi ya wanachama wa ccm wakimvisha mwenyekiti wao mpya mashada ya maua


Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima akimsisitizia jambo fulani mwenyekiti mpya wa ccm mkoa wa mbeya G. Zambi


Mbunge wa Jimbo la Mbozi Mashariki Godfrey Zambi amabaye sasa ni mwenyekiti wa ccm mkoa wa Mbeya akiwashukuru wanachama wa chama hicho kwa kumchagua

WANAFUNZI WASHIRIKI KUNAWA MIKONO


Mwanafunzi wa shule ya Mwenge akimuonyesha mwalimu wake (aliyeshika jagi) namna alivyofundishwa kunawa mikono.

ZAIDI ya Wanafunzi 300 kutoka shule nne za jijini Dar es Salaam, jana waliadhimisha Siku ya Kunawa mikono katika viwanja vya Posta, Kijitonyama, ambayo hufanyika Oktoba 15, kila mwaka huku kwa wanafunzi hao wakiadhimisha jana katika viwanja hivyo.

Wanafunzi hao walikutana katika viwanja hivyo kuanzia saa nne za asubuhi, huku mgeni rasmi akiwa ni Mratibu wa Tiba wa Manispaa ya Kinondoni, Sirila Mwanisi.

Katika maadhimisho hayo, wanafunzi hao walifundishwa jinsi ya kukabiliana na uchafu wakati wote, sambamba na unawaji wa mikono kabla na baada ya kula.

Akizungumza katika viwanja hivyo jana, Sirila alisema, kuwa, ni vyema watu wakajenga utamaduni wa kujitunza kwa wakati wote, ili wakabiliane ba maradhi yanayoweza kuepukika, vikiwano vijidudu vinavyosababisha magonjwa ya tumbo na kipindupindu.

Alisema kwamba watoto wadogo ndio wapo kwenye hatari zaidi, hivyo ni lazima wazazi na walezi pamoja na jamii husika kuwaelimisha kwa ajili ya kuwaweka katika mazingira mazuri.
“Watoto lazima waelimishwe namna ya kunawa mikono kabla na baada ya kula, maana ndio njia pekee ya kukabili vijidudu vya aina mbalimbali, ukiwamo ugonjwa wa kipindipindu ambao ndio hatari zaidi ndani na baadhi ya nchi za Afrika.

“Serikali kwa kushirikiana na asasi mbalimbali tunaamini tutafanikisha usafi wa unawaji wa mikono kwa ajili ya afya njema, ukizingatia kwamba ndio njia ya kufanikisha maisha bora kwa namna moja ama nyingine, hasa wote tukiwa na afya njema,” alisema Sirila.

Maadhimisho hayo ya siku ya kunawa yameandaliwa na Kampuni ya PCB WITNA na kudhaminiwa na sabuni ya Protex kwa ajili ya kukutanisha wanafunzi wa shule za Msingi Shikilango, Kijitonyama Kisiwani, Mapambano, Mwangaza na Mwenge.

Mgeni rasmi ambaye ni Mratibu wa Tiba wa Manispaa ya Kinondoni, Sirila Mwanisi akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Kunawa mikono katika viwanja vya Posta, Kijitonyama, ambayo hufanyika Oktoba 15, kila mwaka huku kwa wanafunzi hao wakiadhimisha siku hiyo jana katika viwanja hivyo.


Wanafunzi ya 300 kutoka shule za Msingi Shekilango, Kijitonyama Kisiwani, Mapambano, Mwangaza na Mwenge wakionyesha mfano wa kunawa mikono mara baada ya kupewa somo.