Subscribe:

search

.

Monday 13 August 2012

MAHAKAMA KUU YAMKATAA MCHUNGAJI GETRUDE RWAKATALE KATIKA USULUHISHI WA KESI YA ASKOFU KAKOBE


MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, imekataa Mchungaji Getrude Rwakatale katika usuluhishi wa kesi ya Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship Church [FBGC], dhidi ya wachungaji wa kanisa lake hilo.
Kakobe anakabiliwa na kesi ya ubadhirifu wa mali na pesa za kanisa hilo zaidi ya Sh14 bilioni na ukikukwaji wa katiba ya kanisa hilo.
Kesi hiyo namba 79 ya mwaka 2011 ilifunguliwa Mei 26 mwaka jana na wachungaji Deuzidelius Patrick, Angelo Mutasingwa na Benedict Kaduma.
Hata hivyo baadaye mchungaji Kaduma aliamua kujitoa katika kesi hiyo kwa ushauri wa ndugu na daktari wake baada ya kupata ajali na kulazimika kufanyiwa upasuaji mkubwa wa kichwa.
Mahakama imepanga kuanza rasmi usuluhishi wa kesi hiyo, Agosti 30, 2012, baada ya kutupilia mbali pingamizi la Kakobe dhidi ya walalamikaji.
Kesi hiyo ilitajwa mahakamani hapo Agosti 6, 2012, ili kuona kama wadaiwa katika kesi hiyo wana pingamizi lolote juu ya Jaji Shangwa kuendelea kuwa msuluhishi, hata hivyo pande zote zilikubali awe msuluhishi wao, ndipo Jaji kuanza rasmi usuluhishi huo Agosti 30, 2012.
Akiahirisha kesi hiyo, Jaji Augustine Shangwa alimtaka Kakobe awepo bila kukosa na kusisitiza kuwaita viongozi wa kidini lakini akaonya kuwa wasiwaite wenye ugomvi na Kakobe huku akimtaja Mchungaji Rwakatale.
“Maaskofu watakaotakiwa ni wale wasio na ugomvi na Kakobe, kwa mfano mkimleta Rwakatale [Getrude] nitamkataa katika kikao. Baada ya kikao nitashangaa kama Kakobe na Wachungaji mtashindwa kumaliza tofauti zenu.”, alitahadharisha Jaji Shangwa.
Jaji Shangwa alisema kuwa mahakama imepewauwezo wa kisheria wa kuzirumbanisha pande mbili zinazoshtakiana na kwamba pia mahakama imepewa uwezo kisheria kuzisuluhisha pande hizo zinazotofautiana.
“Kwa hiyo katika kesi hii tutaanza na hatua ya usuluhishi na ikishindikana tutaanza kuzirumbanisha pande mbili, upande wenu walalamikaji na upande wa Kakobe. Hivyo tutaanza kikao cha usuluhishi  Agosti30 mwezi huu,” , alisema Jaji Shangwa.
Akizungumzia maaskofu ambao wataalikwa kwenye kikao hicho cha usuluhsihi, Jaji Shangwa alisema kuwa kila askofu atakayepata mwaliko wa mahakama aanze kwa kufanya maombi kwanza.
Jaji Shangwa alielezea matumaini yake kuwa mazungumzo hayo yatazaa matunda kwa kuwa wadaiwa wote [ wahusika] katika kesi hiyo ni viongozi wa kiroho.
“Hiyo siku tutaomba maaskofu waombe na kukemea mapepo ili mazungumzo ya usuluhishi yazae matunda. Kwa hiyo naagiza kwamba wahusika wote wawepo bila kukosa na hasa Kakobe.”, alisisitiza Jaji Shangwa.
Awali Askofu Kakobe kupitia kwa Wakili wake Miriamu Majamba, aliwawekea wachungaji hao pingamizi la awali akidai kuwa hati ya madai yao, haionyeshi sababu za madai hayo.
Pia alidai kuwa walalamikaji hao hawana haki ya kisheria, kumfungulia mashtaka  kwa madai kuwa si wachungaji wa kanisa hili na kwamba walikwishafukuzwa na Bodi ya Wadhamini tangu mwaka 2010.
Chanzo;Mwananchi

0 comments: