Subscribe:

search

.

Wednesday 22 August 2012

MAKARANI WA SENSA WALIPWA NA WAJIPANGA KUANZA KAZI




Baadhi ya Makarani wa Sensa wakiwa katika Shule ya Msingi Msisiri Wilaya ya Kinondoni.
Waandishi Wetu
SIKU moja baada ya makarani wa Sensa ya Watu na Makazi kugoma kula kiapo cha utii na kutunza siri, Serikali imewalipa posho zao ili kuendelea na kazi hiyo.

 Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana alisema makarani ambao hawakuwa wamelipwa posho zao, Serikali imeshawalipa na hakuna karani anayedai posho katika wilaya hiyo.

Rugimbana aliyasema hayo jana Dar es Salaam baada ya makarani zaidi ya 800 juzi kutishia kugoma kula kiapo cha utii na kutunza siri kabla ya kulipwa posho zao.  Alisema jana (juzi), kulikuwa na matatizo ya kifedha katika Manispaa ya Kinondoni na ndiyo maana kulikuwa na ucheleweshwaji wa kuwalipa makarani hao posho zao za mafunzo.
“Jana (juzi) kulikuwa na matatizo ya kifedha ambapo Manispaa ilichelewa kupata fedha kutoka hazina, lakini hadi jana asubuhi tulipata fedha hizo na kuwalipa makarani hao posho zao,” alisema Rugimbana na kuongeza:

 “Makarani wote ambao jana (juzi) waligoma kula kiapo tuliwalipa fedha zao na kwamba kinachosubiriwa ni kuanza kwa kazi hiyo,”
alisema.  Alisema kinachotakiwa sasa ni makarani hao kufanya kazi kwa kufuata taratibu zilizowekwa kwani tayari wameshakula kiapo cha utii na kutunza siri zote, sasa ni vyema wakafuata taratibu hizo.

Ofisa Uhusiano wa Manispaa hiyo, Sebastian Mhowera alifafanua kuwa kwa sasa hakuna karani wa Sensa ambaye hajalipwa posho na kwamba kama kuna mtu anatishia kugoma ana sababu zake mwenyewe.
“Manispaa imeshatoa fedha zote na makarani wote wamelipwa posho zao na kama kuna mtu amelipwa tofauti na makubaliano aliyoingia na Serikali aje ofisini kwetu atuambie,” alisema.

 Wakati viongozi hao wa Manispaa ya Kinondoni wakisema hayo jana baadhi ya maeneo ya Mbezi, Kibamba, baadhi ya makarani walitishia kugoma kwa madai ya kutolipwa posho zao. Mwananchi lilishuhudia makarani wakiwa kwenye foleni kwa ajili ya kulipwa posho zao katika vituo vya Shule za Msingi Buguruni na Hekima.
Kwa hisani ya Mwanachi.co.tz

0 comments: