Subscribe:

search

.

Thursday 23 August 2012

MWAKYEMBE AWAWAKIA BANDARI. AMSIMAMISHA MKURUGENZI MKUU WA BANDARI.


Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe akiwatangazia waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana, juu ya kuwasimamisha kwa muda Mkurungenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari (TPA) na Watendaji wengine wa Mamlaka hiyo ili kupisha uchungunzi wa tuhuma mbalimbali katika bandari. Picha na Fidelis Felix
Fidelis Butahe
WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amemsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Ephraim Mgawe, wasaidizi wake wawili na Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Cassian Ng'amilo kupisha uchunguzi wa wizi wa vitu mbalimbali yakiwamo makontena 40 ya vitenge, katika Bandari ya Dar es Salaam.

Dk Mwakyembe alitangaza uamuzi wake huo jana jijini Dar es Salaam, akiendeleza kile alichokifanya Juni 5 mwaka huu alipomtimua kazi aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Paul Chizi.

Hata hivyo, waziri huyo hakutaja majina ya vigogo waliosimamishwa na badala yake alitaja nafasi walizokuwa wakizishikilia ambazo ni pamoja na Meneja wa Kituo cha Mafuta ya Ndege Kurasini (Kurasini Oil Jet - KOJ), Meneja wa Kituo cha Mafuta JET na mhandisi wa mafuta wa kituo hicho, baada ya kubainika kuwapo kwa wizi wa mafuta.

Kutokana na uamuzi huo, Dk Mwakyembe amemteua Mkurugenzi wa Usalama na Mazingira katika Wizara ya Ujenzi, Injinia Madeni Kipande kukaimu nafasi ya Mgawe.

Gazeti hili lilimtafuta Mgawe kwa simu kuzungumzia uamuzi huo, lakini simu yake ya mkononi ilikuwa ikiita muda wote bila majibu na wakati mwingine kukatwa.

Uamuzi huo umekuja baada ya kuwapo kwa taarifa za kupotea kwa makontena takriban 40 ya vitenge na vitu mbalimbali, yaliyokuwa yakipelekwa nchi jirani.

Dk Mwakyembe alisema ameunda kamati ya watu saba ambao hakuwataja majina ili kuchunguza wizi huo na kwamba amewapa wiki mbili tu, wawe wamekamilisha kazi hiyo.

“Nimeunda kamati ya kuchunguza suala hili, nimewapa hadidu za rejea zenye maswali 50..., majina ya waliopo katika kamati hii siyatangazi kwa sasa kwa sababu zangu binafsi,” alisema Dk Mwakyembe.

Alisema amechukua uamuzi huo baada ya kukutana na Bodi ya Wakurugenzi ya TPA juzi na kwamba hawezi kuvumilia kuona nchi inakosa mapato kwa sababu ya wizi uliokithiri.

Alisema kwa muda mrefu katika bandari hiyo ya Dar es Salaam, kumekuwa na malalamiko ya wizi wa vitu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ule wa vifaa vya magari, mafuta na kukithiri rushwa.

Alifafanua kwamba wizi huo umesababisha Bandari ya Dar es Salaam kukimbiwa na wateja ambao hivi sasa wanatumia bandari za Kenya, Msumbiji na Afrika Kusini.

“Makontena yanaibwa kama njugu, hivi sasa watu wa Rwanda, Uganda DRC hawaitumii tena Bandari ya Dar es Salaam, wanaona bora waingie hasara na wameanza kupitisha mizigo yao katika Bandari ya Mombasa Kenya, Beira nchini Msumbiji na Durban Afrika Kusini,” alisema Dk Mwakyembe.

Dk Mwakyembe alisema kuwa hivi karibuni mfanyabiashara mmoja mwanamke alitishia kuhamia nyumbani kwake, baada ya kuibiwa kontena zima la vitenge vilivyokuwa na thamani ya dola 180,000 za Marekani.

“Ni mambo ya ajabu sana hatuwezi kuwa na maendeleo kwa masuala ya ‘kisanii’ kama haya, nimeamua hivi kutokana na mamlaka niliyonayo na uamuzi nitakaouchukua najua wenzangu watanielewa,” alisema.

Wakati akieleza majukumu ya Mamlaka hiyo alisema, “Nimewataka TPA watambue majukumu yao jinsi yalivyo nyeti, nimewaeleza wazi kuwa imani ya wananchi imepungua sana kwa mamlaka hiyo.

“Kama waziri mwenye dhamana sitakuwa tayari kuona jambo hili linaendelea, hili suala haliwezi kuachwa likaendelea ni lazima uchunguzi ufanyike.”

Dk Mwakyembe alisema kuwa ameiagiza bodi ya wakurugenzi, kitengo cha sheria TPA kiuchambue upya mkataba wa Kampuni ya Kupakia na Kupakua Makontena katika Bandari ya Dar es Salaam (Ticts) na kumpatia taarifa Jumatano ijayo.

“Kontena likiwa na vitenge hata ukiweka askari 40 linaondoka, tumepoteza wateja wengi na watu wanaona bora kukimbilia bandari nyingine, nimewaagiza wauchambue upya mkataba huu,” alisema Dk Mwakyembe.

Agizo

Alisema ili kukomesha rushwa ameitaka Bodi ya Wakurugenzi TPA, kuanzia Septemba mosi mwaka huu kuacha kutumia utaratibu wa kulipa fedha dirishani, badala yake fedha zote zilipwe kupitia benki.

“Mtindo wa malipo ya fedha dirishani ndiyo unachochea wizi unaofanywa na mtandao wa kisanii pale TPA. Nimeagiza malipo yote yafanyike kupitia benki au kwa njia zozote za teknohama kuanzia Septemba mosi,” alisema Dk Mwakyembe na kuongeza:

“Kama malipo haya yakiendelea mwezi ujao watakaolipa waandike tu wenyewe barua za kuacha kazi, kampuni ndogondogo nchini zinalipa fedha kupitia benki, kwa nini TPA washindwe?”

Aliongeza kuwa ameiagiza bodi hiyo kuangalia upya mfumo mzima wa uongozi wa TPA na bandari kwa kuwa kuna viongozi wana mamlaka makubwa wakati vyeo vyao ni vidogo.

“Meneja wa bandari ana mamlaka makubwa kiasi kwamba utendaji kazi ndani ya bandari unasuasua wakati wapo viongozi wa juu yake,” alisema Dk Mwakyembe.

Wizi wa mafuta

Akizungumzia wizi wa mafuta, Dk Mwakyembe alisema katika kituo cha KOJ kuna wizi mkubwa wa mafuta ambapo wahusika wakibanwa hutoa kisingizio kuwa mafuta yanayochukuliwa ni machafu.

“Mafuta yale siyo machafu, hiyo imekuwa ndiyo biashara yao kila mwaka, ndiyo maana tenda ya mafuta machafu inagombewa sana, tumefuatilia na kugundua kuwa yanapelekwa katika vituo mbalimbali vya mafuta nchini” alisema Mwakyembe na kuongeza:

“Niliwahi kwenda katika eneo lile saa 12 asubuhi na kukuta malori yanajaza mafuta. Niliuliza lori lina uwezo wa kupakia lita ngapi, kuanzia meneja mpaka watu wa chini kabisa walishindwa kunijibu.”

Alisema kutokana na kitendo hicho, amechukua sampuli ya mafuta hayo na kuyapeleka Mombasa, Kenya kuyapima ili kugundua yana kiwango cha mafuta masafi kwa asilimia ngapi.

Alisema kuwa malori hayo yana uwezo wa kupakia lita 26,000 za mafuta lakini wahusika wanadai kuwa yanaweza kupakia lita 9,000 tu.

“Mafuta haya huibwa wakati yakitolewa katika meli na kupelekwa katika magari, karibu asilimia mbili nzima ya mafuta huibwa, kiwango ambacho ni kikubwa sana,” alisema.

Alisema kutokana na hali hiyo ameagiza kurejeshwa kwa kifaa cha kupimia wingi wa mafuta katika malori ya mafuta, ndani ya mwezi mmoja kuanzia jana.

Aanika ufisadi

Alisema kampuni ya Singirimo iliyopewa zabuni ya kusafirisha mafuta machafu, mkataba wake ulishaisha siku nyingi, lakini bado inaendelea na kazi hiyo na kwamba mwaka 2008, Ikulu iliwahi kueleza kuwa kampuni hiyo ni kinara kwa kusafirisha mafuta masafi na kudai machafu.

“Kampuni hii kila mwaka inashinda tenda ya kusafirisha mafuta tu, hivi sasa inachunguzwa na Ewura na Takukuru, nimeagiza mamlaka husika kwamba kampuni hii isijihusishe tena na usafirishaji wa mafuta ili kupisha uchunguzi,” alisema Dk Mwakyembe na kuongeza:

“Kampuni iliyokuwa namba mbili katika utoaji wa tenda ndiyo ipewe jukumu hilo na kama isipopewa ndiyo nitajua kuna kitu kinaendelea.”

Alisema kuwa mwaka 2008 Ikulu ilisema kuwa kampuni ya Singirimo ni ya wafanyakazi na vigogo wa TPA na inasafirisha mafuta masafi na kudai kuwa ni machafu
Chanzo:Mwananchi.co.tz

0 comments: