Subscribe:

search

.

Monday 20 August 2012

TAARIFA YA M4C MOROGORO


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetangaza mafanikio kiliyopata katika majimbo sita (na nusu) ya Mkoa wa Morogoro katika operesheni kinayoendesha mkoani humo, huku pia kikitoa tuhuma nzito dhidi ya mahasimu wao wa kisiasa CCM kwa kuendesha na kusimamia hujuma dhidi ya chama kikuu hicho cha upinzani nchini.


Katika mkutano na waandishi wa habari jana Mjini Morogoro, CHADEMA kimesema kuwa kwa kutumia Operesheni Sangara-Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) inayoendelea mkoani humo, kimefanikiwa kufika katika kata 195 kati ya kata 137 za mkoa mzima wa Morogoro, ambapo kimefanya mikutano katika vijiji 471 ambapo wananchi wamekichangia takriban milioni 17.8 katika mikutano hiyo.

Mbali ya takwimu hizo, chama hicho kimesema kuwa katika siku 13 (hadi jana) katika mkoa huo kimeweza kuvuna wanachama wapatao 31,537, kimeunda matawi ya kudumu zaidi ya 100, mapato ya mauzo ya kadi yakiwa ni Tshs. Milioni 15.7, huku pia kikikabidhiwa takriban kadi 7650 za vyama vingine kutoka kwa Watanzania ambao waliamua ‘kuvua gamba na kuvaa gwanda’ katika mikutano ya hadhara ya chama hicho

Pia chama hicho kimetoa tamko la kuwataka Watanzania wote bila kujali tofauti zao katika jamii kushiriki katika shughuli ya sense ya watu na makazi, kikisema kuwa ni muhimu idadi ya watu kujulikana na kuelewa namna wanavyoishi na kupata huduma za kijamii ili iwe rahisi kuweza kupanga mipango mbalimbali, huku kikisema kuwa idadi hiyo ya watu itakisaidia pia chama hicho kikishika dola kama kinavyojiandaa sasa.

Kauli dhidi ya hujuma

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari jana, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Willibrod Slaa alitoa tuhuma nzito dhidi ya CCM kuwa kimekuwa na mtindo wa kuingiza silaha nchini, zikiwemo bunduki bila kibali wala kuzikatia leseni, kisha kinawapatia vijana wake wanaowekwa kwenye makambi maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kufundishwa mbinu za kuwashughulikia wapinzani wao kisiasa, hasa CHADEMA.


“Kwa hapa Morogoro Mjini tayari tunazo taarifa tumeshaambiwa kuna vijana kama 10-20 wanaandaliwa kufanya njama za kuhujumu CHADEMA, watavalishwa kombati kama hizi za kwetu, watafanya fujo ili ionekane ni sisi, wamepewa sumu, tindikali na sindano kwa ajili ya kukamilisha hizo hujuma wanazopanga dhidi yetu. Kwa baadhi yetu tunaowafahamu CCM hili si suala jipya, walifanya hivyo hivyo wakati wa uchaguzi mdogo Igunga, moja ya makambi ilikuwa Ilemo, Iramba.


“Lakini pia huu ndiyo mtindo wao, wana tabia ya kuingiza hata bunduki nchini bila kibali wala leseni wanapatia vijana, kisha wakishafanya hivyo wanajiandaa kuhamishia tuhuma CHADEMA, hii ndiyo sababu ya Wilson Mkama kutamka wakati ule kuwa tumeingiza makomandoo nchini, kumbe wao tayari wameshaweka vijana makambini na wanafundisha, tena waliohusika kufundisha ni polisi na usalama wa taifa. Tulitoa taarifa polisi juu ya masuala yote na ushahidi tukawapatia wafuatilie, lakini kwa sababu wanahusika mpaka leo hakuna hatua yoyote.

Mbali ya kutoa onyo kwa mtu yeyote ambaye anajipanga kukihujumu chama hicho katika opresheni hiyo inayoendelea mkoani Morogoro kabla ya kuelekea Iringa, Dkt. Slaa alisema kuwa watatoa taarifa polisi juu ya njama hizo za vijana kuandaliwa lakini hawana mpango wowote wa kushtaki CCM kwa njama zote wanazozibaini kuwa zinalenga kukihujumu chama hicho, kwani kufanya hivyo ni ‘sawa na kupeleka kesi ya nyani kwa ngedere’. Lakini alisistiza kuwa wakati utakapofika wataweka hadharani nyaraka ya baadhi ya alizodai kuwa ni njama zinazoendeshwa na CCM dhidi yao.


Tamko dhidi ya Pinda

Mbali ya hilo, Dkt. Slaa pia alisema kuwa CHADEMA kinatoa muda wa mwezi mmoja kwa Ofisi ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kutoa ufafanuzi wa kina na hadharani juu ya michango yote ambayo Watanzania walichangia katika maafa ya mafuriko ya Kilosa, Dar es Salaam, mabomu ya Gongolamboto na Mbagala, huku pia akimtaka Pinda amwagize CAG afanye ukaguzi wa harufu ya matumizi mabaya katika maafa hayo, akitolea mfano wa Kilosa ambako alisema wamebaini mambo mengi yasiyokuwa ya kawaida.


Dkt. Slaa pia aliongeza kusema kuwa wanafanya utaratibu ili chama hicho kiwaagize wabunge wa chama hicho waandae hoja mahsusi kisha ipelekwe bungeni ili kuihoji na kuitaka serikali itoe taarifa ya kina ya hali ilivyo katika maeneo yote hayo yaliyopatwa na maafa, akisema kuwa wamebaini kuwepo kwa ufisadi mkubwa katika michango ya waathirika wa matukio ya maeneo hayo, huku ahadi walizoahidiwa na serikali hazijatimizwa mpaka leo, ndiyo maana bado kuna malalamiko kutoka kwa watu.

Mbali ya hilo pia amemtaka Waziri Mkuu Pinda kutoa taarifa ya kina juu ya namna gani mpaka sasa serikali imefanyia kazi migogoro ya wakulima na wafugaji katika maeneo mbalimbali ikiwemo Kilosa na Rukwa kama alivyowahi kuahidi bungeni kuwa serikali italifanyia kazi tatizo hilo ili kuepusha maafa ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara kila mara makundi hayo yanapoingia katika mikwaruzano ya kugombea maeneo ya kazi zao za kilimo au kuchungia mifugo yao.

“Wakati huo nikiwa bado bungeni, Pinda alituomba kuwa tutulie serikali itatoa kauli juu ya suala hili, kesho yake akatuahidi kupitia kwa Waziri Celina Kombani wakati huo akiwa TAMISEMI kuwa watalifanyia kazi tatizo la wafugahi na wakulima, lakini leo hii wanayofanyiwa wafugaji wa Kilosa kwa mkono wa serikali kufanywa mtaji wa viongozi kwa kuombwa rushwa baada ya kukamata wake zao wengine wana mimba au mabinti zao, hakiwezi kuvumilika. Miaka mitatu ameshindwa kushughulia tatizo hili, wakulima na wafugaji wanateseka, kwa nini asiwajibike kwa kujiuzulu,” alisema Dkt. Slaa.

“Tumekutana na waathirika wa Kilosa, kwa kweli wanaishi katika hali ambayo hutegemei binadamu anaweza kuishi, watu wale wametelekezwa na serikali, wakati wanapata matatizo hayo katika Ofisi ya Waziri Mkuu kuna kitengo cha maafa ambacho kila mwaka kinapangiwa bajeti kwa kazi hiyo, lakini mbali ya hilo, Watanzania nchi nzima walihamasika kuwachangia waathirika hao, lakini mpaka sasa nia ajabu michango hiyo walikuwa wakiisikia redioni na kuiona kwenye televisheni, tunamtaka Pinda atuambie.

“Tunataka uwajibikaji wa serikali katika namna ambavyo waathirika wa majanga au maafa haya wamesaidiwa kama binadamu na Watanzania wanaolipa kodi kwa serikali kila siku, tena mkikumbuka yale ya Gongolamboto na Mbagala yalitokana na uzembe wa serikali kabisa, sasa hatuwezi kuona watu wanaendelea kuumia kwa uzembe wa serikali,” alisema Dkt. Slaa.

Tamko la Sensa

Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Zanzibar, Said Issa Mohamed aliwataka Watanzania wote nchini bila kujali tofauti zao za kidini wala rangi au maeneo, kushiriki shughuli ya sense ya watu na makazi itakayofanyika mwishoni mwa juma hili. Akitoa wito huo, aliongeza kusema kuwa ushiriki wa wananchi katika zoezi hilo muhimu katika kupanga mipango ya maendeleo, hasa katika utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii utakisaidia chama hicho pia katika harakati za kuwapigania.


“Hata baba ndani ya nyumba ukijua idadi ya watu wako katika familia ni rahisi kuweza kupanga mahitaji yao, lakini mbali ya hilo Watanzania wanajua namna ambavyo takwimu hizi zitatusaidia sisi CHADEMA tutakapoingia madarakani kama mabvyo tunajipanga kutokana na wao kuendelea kutukubali na kutuunga mkono, kwetu CHADEMA ukijua watu na makazi yao itakuwa rahisi kujua mahitajio ya wananchi na kuweka mfumo sahihi wa kuwatumikia,” alisema Mohamed.


Mafanikio ya Operesheni Morogoro


Naye Kamanda wa Operesheni Sangara-M4C inayoendelea mkoani Morogoro, Benson Kigaila akizungumzia mafanikio na changamoto tangu waanze, ambapo jana ilikuwa ni siku ya 13 tangu uzinduzi katika mkoa huo ulipofanyika Wilayani Kilombero, mjini Ifakara, alisema kuwa kwenye mkutano wa mwisho kwa mkoa wa Morogoro utakaofanyika kati ya Alhamis au Ijumaa wiki hii, wataweka hadharani ‘mali’ zote za vyama vingine walizokabidhiwa na waliokuwa wanachama wa vyama hivyo ambao wamehamia CHADEMA.


“Leo ni siku ya 13 tangu tumeanza operesheni hii kwa mkoa wa Morogoro, safari hii iliyoanzia Morogoro itatuchukua katika mikoa mitano, Iringa, Dodoma, Manyara kisha Singida. Hadi sasa tumekwenda majimbo sita na nusu ya Morogoro kwa sababu tumepiga nusu ya Mvomero na nusu tutaimalizia kesho. Katika siku zote hizi wananchi wameendelea kutuchangia katika mikutano yao, wametoa michango ya hali na mali, ni ishara nzuri ya kuwa wanaunga mkono mabadiliko na wanashiriki kumiliki mchakato huu muhimu.


“Kutokana na ziara hii kutwa tofauti sana na zingine za huko nyuma, inafanana fanana na ile ya Kusini, wanachama wote wanasajiliwa, uongozi unaundwa kwa kila tawi, tuna namba zao za simu, kwa hiyo hata tukiamua kuwasiliana nao kwa meseji kwa mara moja tunaweza kufanya hivyo nchi nzima, tunaunda mtandao wa kudumu wa chama kinachojiandaa kuchukua dola. Katika mikutano hiyo tumepokea kero za wananchi, tumezungumza nao, wameonesha matumaini makubwa sana kwetu,” alisema Kigaila.


Baada ya mapumziko ya siku mbili kwa ajili ya Siku Kuu ya Eid-El-Fitr, chama hicho kitaendelea na operesheni yake katika mkoa wa Morogoro leo, kwa kumalizia Jimbo la Mvomero

0 comments: