Subscribe:

search

.

Sunday 12 August 2012

WARIOBA AVILAUMU VYAMA VYA SIASA KWAMBA VINAINGILIA UHURU WA WANANCHI KUTOA MAONI YA KATIBA MPYA

Fidelis Butahe
JULAI 2 mpaka 30 mwaka huu Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilikuwa ikikusanya maoni ya wananchi kuhusu Katiba mpya katika mikoa minane ya Tanzania bara na visiwani.

Awamu ya kwanza ya ukusanyaji wa maoni ya wananchi ilifanyika katika mikoa ya Pwani, Dodoma, Manyara, Kagera, Shinyanga, Tanga, Kusini Unguja na Kusini Pemba na litaendelea katika awamu ya pili kuanzia Agosti 27 mwaka huu.

Wananchi waliohudhuria katika mikutano hiyo ni 188,679 ambapo 46,620 waliweza kutoa maoni yao, huku 17,440 wakitoa maoni kwa njia ya kuzungumza na 29,180 kwa njia ya maandishi.

Kwa idadi hiyo, maana yake ni kwamba katika mkutano mmoja ulikuwa ukihudhuriwa na watu 489.

Pamoja na kukumbana na changamoto mbalimbali, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji mstaafu Joseph Warioba anasema tatizo kubwa walilokumbana nalo katika zoezi hilo ni vitendo vya vyama vya siasa kuwaelekeza wananchi mambo ya kuzungumza.

Anasema mbali na vyama vya siasa hata Asasi za Kiraia, wanaharakati na mashirika ya dini nayo yamekuwa na tabia hiyo na anayataka kuacha tabia hiyo kwa kuwa inawanyima watanzania uhuru wa kuzungumza.

“Vyama vya siasa vinaingilia uhuru wa wananchi wa kutoa maoni, vimekuwa vikitoa kauli na maelekezo kwa wanachama wao kufuata msimamo wa vyama husika jambo ambalo linawanyima wananchi uhuru” anasema Jaji Warioba na anaongeza;

“Tunavitaka vyama vya siasa pamoja na asasi za kiraia, mashirika ya dini na wanaharakati kuacha tabia hii, wawaache wananchi watoe maoni yao kwa sababu tumepata waraka wa vikundi hivi vya kijamii unaowabana wananchi.”

Anasema kuwa katika zoezi la ukusanyaji wa maoni, Tume hiyo iliona nyaraka mbalimbali za vyama na asasi hizo, vinavyowaelekeza wananchi mambo ya kuchangia mbele ya Tume hiyo.

Anasema kuwa sheria ipo wazi kwamba makundi hayo yakitaka kutoa elimu kwa wananchi yanatakiwa kutoa taarifa kwa Tume.

Anasema kwamba hata vikipewa nafasi hiyo viitumie vyema na sio hiyo kuwapangia wananchi cha kuzungumza.

“Kuna baadhi ya maeneo wananchi walikuwa wakitakiwa kutoa ufafanuzi wa kile walichokizungumza walishindwa, hii ni kwa sababu waliambiwa cha kuzungumza,” anasema Jaji Warioba.

Anasema kuwa makundi hayo nayo yatakuwa na muda maalum wa kutoa maoni yao na kwamba kwa sasa wameshaanza kuchukua maoni ya vyombo vya ulinzi na usalama katika mikoa minane.

Yaliyosemwa na wananchi

Jaji Warioba anasema moja ya mambo yaliyozungumzwa sana na wananchi wakati wakitoa maoni ya Katiba mpya ni pamoja na mfumo wa Uongozi na Utawala.

Anasema wananchi walihoji madaraka aliyonayo Rais katika uteuzi wa nafasi mbalimbali zikiwamo za watendaji wakuu wa taasisi za serikali.

“Wananchi walihoji uteuzi wa nafasi mbalimbali ndani ya serikali likiwamo suala la uteuzi wa wakuu wa mikoa, wilaya na watendaji wengine wa serikali,” anasema Jaji Warioba.

Jaji Warioba anasema pamoja na kuwa wananchi walio wengi hawaijui Katiba lakini ni makosa kudhani kuwa wananchi hawajui kitu, kwani waliweza kueleza kwa kina mambo yanayowagusa na
yale yanayowahusu.

“Ukiwasikiliza utabaini kuwa walikuwa wakizungumzia mwelekeo wa Sera na Serikali, walikuwa wakizungumzia Haki za Binadamu na pia kwa uwazi zaidi walieleza ni Tanzania gani wanayoitaka.

Anasema mambo mengine ambayo wananchi hao walitaka yaingizwe katika Katiba Mpya ni pamoja na masuala ya ardhi, kilimo, elimu, huduma za afya, hifadhi za jamii, nafasi ya utoaji wa haki na madaraka ya wananchi.

Anasisitiza licha ya kuwa Watanzania wengi hawaijui Katiba ya sasa lakini maoni waliyoyatoa yanaendana na vifungu vilivyomo katika Katiba hiyo.

Anafafanua kwamba licha ya kuwa muda wa miezi 18 ambayo Tume hiyo imepewa ni mchache, lakini wameipokea hiyo kama changamoto na wamejitayarisha kuifanyika kazi na kuhakikisha kuwa uchaguzi wa mwaka 2015 utafanyika huku kukiwa na Katiba mpya.

“Tunapenda sana uchaguzi wa 2015 ufanyike wakati nchi ikiwa na Katiba mpya na lazima tufanye kazi hii ndani ya muda uliopangwa,” anasema Jaji Warioba.

Walemavu

Anasema kutokana na kutambua haki za wenye ulemavu wa kuona, kusikia na kuzungumza, Tume hiyo imefanya mawasiliano na vyama vyao ili kupata njia sahihi ya kuwashirikisha katika utoaji wa maoni.

“Juhudi hizi ni pamoja na kuwapatia vitabu maalum ili waweze kusoma na kupata mwanga wa mambo watakayoweza kuchangia,” anasema Jaji Warioba.

Anasema kuwa katika mikutano iliyopita, Tume ililazimika kutafuta watu na kuwalipa ili waweze kuwa wakalimani wakati ambapo wasiosema na kusikia wanapotaka kutoa maoni yao.

Aidha Jaji Warioba anasema hata wale walio nje ya nchi wanaweza kutoa maoni kupitia Tovuti ya Tume hiyo na kwamba mpaka sasa bado hawajapata njia sahihi ya kuchukua maoni ya wafungwa.

Anaongeza kuwa kutokana na waumini wa dini ya Kiislamu kuwa katika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, kuwapo kwa zoezi la Sensa ya watu na makazi, Tume hiyo imeamua kusogeza mbele tarehe ya ukusanyaji wa maoni, itaendelea na zoezi hilo kuanzia Agosti 27 mwaka huu.

Anasema kuwa katika awamu ya pili ya ukusanyaji maoni, Tume itakwenda katika mikoa ya Lindi, Mwanza, Kigoma, Mbeya, Katavi, Morogoro na Ruvuma.

Muungano
Kuhusu Muungano, Jaji Warioba amesema wananchi wana mawazo tofauti, wapo waliosema wanataka Muungano wa Serikali tatu, wako wanaotaka wa Serikali mbili, wapo waliosema wanataka Muungano wa Mkataba na wapo waliosema hawataki kabisa Muungano.
“Haya yote ni mawazo tuliyoyapokea na tutayafanyia kazi, hivi sasa hatuwezi kutoa ufafanuzi wowote kuhusu suala la Muungano, lakini tunaendelea kupokea maoni, tutayachambua, tutawarudishia tena wananchi wayahakiki kabla ya kuandika rasimu…”

Chanzo:www.mwananchi.co.tz

0 comments: