Subscribe:

search

.

Friday 10 August 2012

WAVUVI 9 WAMEDAIWA KUUWAWA KWA RISASI NA ASKARI WA HIFADHI YA TAIFA RUBONDO

Na Mwandishi Wetu, Geita


WAVUVI 9 wanadaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi na askari wa doria wa Hifadhi ya Taifa ya Rubondo, mkoani Geita. Habari za kuaminika zilizopatikana kutoka Rubondo, zinasema mauaji hayo, yamefanywa siri kubwa kwa sababu viongozi wa Jeshi la Polisi wamegoma kutoa maelezo.

Mbali ya watu hao kupigwa risasi, habari zinasema askari hao, waliwachukua wavuvi wengine ambao idadi yao haijajulikana na kuwatupa sehemu ya kina kirefu cha maji, kwa kutumia boti ziendazo kasi.

Kutokana na hali hiyo, uongozi wa Chama cha Wananchi (CUF), Wilaya ya Geita, umemwandikia barua Mkuu wa Wilaya hiyo, Omar Manzie, kulaani tukio hilo.

Katibu wa CUF Wilaya ya Geita, Seveline Malugu, aliwaambia waandishi wa habari kuwa matukio ya aina hiyo, yalitokea mwishoni mwa mwaka jana na mwanzoni mwa mwaka huu.

“Tumeamua kumwandikia barua mkuu wa wilaya yetu, Omari Manzie kumwelezea unyama huu, unaofanywa na baadhi ya askari wa kisiwa hiki…tunamtaka atoe ufafanuzi juu ya matukio ya mauaji ya watu 9 yaliyotokea jirani na hifadhi hiyo ndani ya Ziwa Victoria,” alisema Malugu.

Alisema askari hao, waliwakamata baadhi ya wananchi ambao ni wavuvi karibu na mpaka wa hifadhi ya kisiwa hicho, kisha kuwaua na wengine kuwabambikizia kesi.

Alisema katika taarifa ya maandishi waliyotuma kwa DC Manzie, wamewataja baadhi ya watu waliopigwa risasi na kutoswa majini, kuwa ni Paschal Mabwete, Selemani Tembo, Jeremiah Mussa, Abel Zacharia na mtu mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Kulwa.

Wengine ni Idd Mussa, Shija Shigondo, Baluhya Buzinza na Marco Masanyiwa.

Alisema katika tukio hilo, watu wawili walinusurika kifo baada ya kufanikiwa kuogelea hadi nchi kavu, mmojawapo ni Burhan, mkazi wa kisiwa cha Ikuza wilaya ya Muleba mkoani Kagera.

Mkuu wa Kikosi cha Doria cha Hifadhi hiyo, aliyejitambulisha kwa jina la J. Chuwa, alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusu matukio hayo, alisema hawezi kuyatolea ufafanuzi wowote kwa kuwa alikuwa safarini.

“Nipo safarini jamani, nawaomba mumtafute Mkuu wa Hifadhi awaelezea tukio hilo,” alisema Chuwa.

Akizungumza na MTANZANIA, mmoja wa wananchi waliofanyiwa unyama huo, ambaye hakutaka jina lake liandikiwe gazetini, alisema Aprili 26, mwaka huu, alipokea taarifa kwa njia ya simu kuwa rafiki zake wamekamatwa na askari wa kisiwa hicho.

Alisema askari hao, waliomba wapewe Sh 100,000 kutoka wavuvi hao kama faini ya kuvua samaki eneo la hifadhi, ili wawaachie.

“Tuliwasiliana na mwajiri wa wavuvi, waliamua kuchukua boti na kiasi hiki cha fedha, lakini jambo la kusikitisha ni baada ya kubaini kuwa mwajiri huyo ana Sh 600,000 mfukoni askari walimwamuru awapatie zote.

“Walinipokonya fedha zangu zote, nilipowahoji waliamua kunichukua hadi kwenye kambi mojawapo iliyopo ndani ya hifadhi hiyo na kuanza kunishambulia kwa vipigo vikali…kisha kunibambikizia kesi ya kuingia ndani ya hifadhi pasipo kibali cha Serikali, kukutwa na nyavu haramu na kutuhumiwa kutoa rushwa ili askari wasifanye kazi,” alisema mwajiri huyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Leobard Paul, alipoulizwa na MTANZANIA, kuhusiana na madai hayo alijibu kwa kifupi, “nasema tukio hilo hatuna, kama lingekuwepo ningetoa taarifa”.

Juhudi za kumpata Mkuu wa Wilaya, Omar Manzie, ili kutafuta ufafanuzi wa tukio, hakupatikana baada ya simu yake ya kiganjani kutokuwa hewani.
Chanzo: Mtanzania

0 comments: