search

.

Wednesday, 15 August 2012

ZITTO ADAI SAKATA LA RADA BADO BICHI MNONa. Zitto Kabwe.
Hiii ni sehemu ya 2.5 katika hotuba ya Waziri Kivuli na Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Wizara ya Fedha na Uchumi Mh Kabwe Zuberi Zitto kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2012/2013.
2.5 MKOPO WA KUNUNUA RADA ILIYOGUBIKWA NA UFISADI
Mheshimiwa Spika, sehemu ya Malipo ya Deni la Taifa ni Mkopo ambao Serikali ilichukua ili kununua Rada kutoka kampuni ya BAE ya Uingereza.
Suala hili la rada limejadiliwa sana nchini kwa upande mmoja tu wa ufisadi wa kupandisha bei ya Rada na hatimaye kurejeshwa kwa iliyoitwa chenji ya Rada.
Hiyo ilikuwa ni nusu tu ya ukweli kuhusu suala la Rada kwani Serikali ilikopa kiasi cha dola za kimarekani 40 milioni kutoka Benki ya Barclays ya Uingereza kwa ajili ya kununulia Rada.
 Mkopo huo ulikuwa na Riba ya asilimia 4.9 juu ya kiwango cha riba zinazotolewa na Benki ya Dunia au IMF.
Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kujua kama mkopo huu umeshalipwa wote na jumla tulilipa kiasi gani cha fedha.
Ukilinganisha fedha iliyorejeshwa kama chenji ya Rada na Fedha ambayo Tanzania iliilipa Benki ya Barclays (Principal amount and Interest), je chenji ya Rada ilikuwa na thamani yoyote kifedha? 
Mjadala wa ununuzi wa Rada hauwezi kuisha kwa kufurahia kurejeshewa chenji tu.
Mjadala huu bado mbichi kabisa kwani tunataka ukweli na ukweli mtupu uelezwe kwa umma na kuona Taifa lilipata hasara kiasi gani kwa ufisadi huu wa kimataifa na hatua stahiki za kisheria kuchukuliwa dhidi ya wote walioingiza hasara kwa Taifa letu.

0 comments: