Subscribe:

search

.

Thursday 4 October 2012

Mujjahidina wavamia makaburi Mkoani Pwani wakitaka Kaburi la Aruina Rolan Lifukuliwe


NA MWANDISHI WETU, BAGAMOYO

KUNDI la waumini wa dini ya Kiislamu (Mujjahidina), kutoka Msikiti wa Majani Mapana Tandika, wilayani Bagamoyo, mkoa wa Pwani, limefanya vurugu kubwa baada ya kuvamia makaburi ya Kiislamu na kutaka kaburi alilozikwa mtoto Aruina Rolan Mitaban lifukuliwe.

Waislamu hao, ambao walionekana kujawa na jazba, walidai mwili wa mtoto huyo, hauruhusiwi kuzikwa katika maeneo yao, kwa sababu ni Mkristo.

Tukio hilo lilitokea Septemba 30, mwaka huu, ikiwa ni mwezi mmoja baada ya kuzikwa kwa mwili wa mtoto huyo, katika makaburi hayo.

Tukio hilo, limeonekana kuibua hisia kali kwa wakazi wa Bagamoyo, ambao miongoni mwao walidai huo ni unyama wa kupindukia.

“Haiwezekani kaburi la mtoto kama yule, malaika wa Mungu asiyejua kitu, linakwenda kufukuliwa kinyama vile… nadhani tunakoelekea ni kubaya sasa,” alisema Suleiman Wahid.

“Huwezi kusambaratisha kaburi namna hii, ilitakiwa wakutane na viongozi wa makaburi kwanza, marehemu yule ana kosa gani? Watanzania tunapotea,” alisema Wahid.

Kufuatia tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Ahmed Kipozi, aliamua kuitisha kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama cha dharura ili kujadili.

Baada ya kuitisha kikao hicho, aliziita pande mbili zinazohusika, ili kupata ufumbuzi wa suala hilo.

Kipozi aliwataka waumini wa dini hizo na wakazi wa wilaya hiyo, kujenga tabia ya kuvumiliana pale kunapokuwa na matatizo, badala ya kuendekeza jazba na hasira ambazo haziwezi kuleta tija.

Mara baada ya kikao hicho cha kamati ya ulinzi na usalama, upande wa marehemu huyo wakiongozwa na baba wa marehemu, Rolan Mitaban, Oktoba 2, mwaka huu walilazimika kwenda kufukua mwili huo wa marehemu na kwenda kuuzika upya jijini Dar es Salaam.

“Tukio hili limetokea, nikalazimika kuitisha kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama, na pande zote zinazohusika.

“Moja ya maazimio tuliyokubalina ni kwamba, kaburi lile lisibughudhiwe na mtu yeyote na ndugu zao walijengee kama yalivyojengewa makaburi mengine.

“Lakini katika hali ya kushangaza, nimesikia jana baba mzazi wa marehemu akiwa na ndugu zake, waliamua kwenda kufukua mwili wa marehemu na kwenda kuuzika Dar es Salaam,” alisema Kipozi.

Kutokana na tukio hilo, DC Kipozi alitoa wito kwa viongozi wa dini, kuhakikisha wanawasiliana na ofisi yake, ili kushughulikia matatizo ya aina hiyo yanapojitokeza, ili kuepusha madhara ambayo yanaweza kutokea.

Baadhi ya ndugu wa marehemu, ambao waliomba majina yao yahifadhiwe, walisema kitendo kilichofanywa na waumini wa dini ya Kiislamu si cha kiungwana, kwani kama kulikuwa na tatizo hilo, walipaswa kuwataarifu wahusika ili waweze kwenda kushughulikia kwa kufuata sheria.

Hii ni mara ya pili kutokea kwa vurugu katika makaburi ya Tandika, itakumbukwa mwanzoni mwa mwaka huu, kuliibuka uvumi kuwa kuna joka kubwa la kishirikina katika makaburi hayo na kupelekea mganga wa kienyeji maarufu Zoazoa, kwenda kuweka matambiko ambayo hayakuzaa matunda.
Chanzo: Mtanzania

0 comments: