search

.

Friday, 5 October 2012

NINI KINAENDELEA KATI YA SUMAYE NA LOWASA. FUATILIA HAPA.
MGOGORO unaodaiwa kumuhusisha Waziri Mkuu mstaafu, Bw. Frederick Sumaye na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Bw. Edward Lowassa, umechukuwa sura mpya kwa kile kinachoonekana 
kila mmoja kumtupia mpira mwenzake.

Juzi gazeti hili lilimpigia simu Bw. Lowassa ili aweze kuzungumzia madai yanayodaiwa kutolewa dhidi yake na Bw. Sumaye, kupitia gazeti moja (si Majira), linalotoka kila siku.

Pia gazeti hili lilimpigia simu Bw. Sumaye kutaka ufafanuzi wa madai yake kwa Bw. Lowassa lakini aliahidi kuzungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam siku chache zijazo.

“Nitawaita waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ili nizungumze kila kitu kuhusu uchaguzi wa NEC, Hanang',” alisema Bw. Sumaye.

Gazeti hilo lilidai, Bw. Sumaye ametangaza vita na Bw. Lowassa kama atawania urais 2015 kwa tiketi ya CCM. Katika majibu yake, Bw. Lowassa alisema yupo kijijini hivyo hafahamu chochote.

Alisema yeye mwenyewe amezisikia taarifa hizo lakini hajalisoma gazeti hilo hivyo hana majibu na kuahidi kutoa ufafanuzi wa madai hayo kesho yake (jana), baada ya kusoma gazeti.

Jana gazeti hili lilimpigia siku Bw. Lowassa ambaye alidai; “Nimesoma magazeti, nimeona walionukuliwa walikuwa ni wasaidizi wake, namsubiri azungumze yeye mwenyewe ili nimjibu. 

“Nimesikia leo (jana) kuwa atazungumza na waandishi wa habari, tusubiri azungumze halafu nitamjibu,” alisema Bw. Lowassa.

Alipotakiwa kuzungumzia mgogoro huo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Bw. Nape Nnauye, alisema unawahusu watu wawili hivyo asingependa chama hicho kihusishwe.

“Waulizeni wao wenyewe msikihusishe chama ambacho hakihusika na mgogoro huo,” alisema Bw. Nnauye.

Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Bw. Augustino Mrema alipotakiwa kufafanua mgogoro huo unaweza kuiathiri vipi CCM alidai ni wa kimasilahi na kisiasa.

“Watanzania hawawezi kugawanyika kwa sababu ya mgogoro wa Bw. Lowassa na Bw. Sumaye, tusiwe wajinga wakati wenzetu wanalima, ndugu wakigombana, wewe chukuwa jembe ukalime.

“Kimsingi tunapaswa kuwa macho, tusije kutekwa na mkondo huo, hizo ni siasa za kujipanga, hao ni ndugu wawili hivyo Watanzania wanapaswa kuendelea na shughuli zao za kimaendeleo,” alisema.

Alisema viongozi hao wastaafu wanataka madaraka hivyo wanachokifanya si jambo geni..na majira

Chanzo: Majira

0 comments: