Subscribe:

search

.

Friday 17 August 2012

DR ULIMBOKA AFUNGUKA



KIONGOZI wa madaktari, Dk Stephen Ulimboka amewataka watanzania wasiwe na hofu na wasubiri siku maalum ambayo ataweka wazi ukweli wote kuhusu namna alivyotekwa na kuteswa, pia hali yake ya kiafya kwa sasa.
Dk Ulimboka ambaye amerejea nchini hivi karibuni kutoka Afrika Kusini alikokuwa amepelekwa kwa ajili ya matibabu alisema jana kuwa hawezi kuzungumza lolote kwa sasa  na aachwe apumzike kwani ameugua na ametengana na familia yake kwa muda mrefu, hivyo anahitaji muda wa kuwa peke yake.
“Niacheni nipumzike kwa sasa. Wakati muafaka ukifika, nitasema yote. Sitaacha kusema, muda muafaka ukiwadia nitayasema yaliyonitokea na taratibu maalum zitaandaliwa ili nizungumze na watanzania,” alisema Dk Ulimboka.
Alisema hawezi kuzungumza bila utaratibu maalum bali atazingatia taratibu zitakazoandaliwa na uongozi wa Jumuiya ya Madaktari (MAT) ndipo ataueleza umma na kusema  yaliyo moyoni kuhusu kutekwa na kupigwa kwake.
“Haya mambo yatawekwa hadharani lakini ni kwa utarartibu maalum, si kama hivi mnavyotaka ninyi. Kila mtu ananiuliza halafu mnakwenda kuandika ya kwenu, naona hii imekuwa kama biashara sasa,” alisema.
Aidha Dk Ulimboka alivilaumu baadhi ya vyombo vya habari kwa  kuandika habari ambazo si za kweli kuhusu suala la kutekwa na kuteswa kwake na kusema kuwa wamekuwa wakipotosha ukweli wa tukio lenyewe.
“Wengine wananipigia simu na kunijulia hali, nikiwaambia basi wanaenda kuandika tofauti, kwa mfano juzi wameandika kuwa nimeonekana nikipanda boti, jambo ambalo si la kweli,” alisema.
Akizungumzia hilo, makamu wa rais wa MAT, Prinus Saidia alisema Dk Ulimboka kwa sasa yupo mapumzikoni na atazungumza kwa kina baada ya muda mfupi.
Alisema madaktari wamekubaliana kuwa Dk Ulimboka aachwe apumzike baada ya kipindi kigumu cha muda mrefu lakini atazungumza kwa undani wakati ambao utakubaliwa na jumuiya hiyo.
Wakati huo huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Haki za Raia, Siasa na Mwenendo wa Bunge, Marcossy Albanie amesema  ataitisha mkutano wa waandishi wa habari siku ya Jumatatu ambapo pamoja na mambo mengine atazungumzia suala la kutekwa na kuteswa kwa Dk Ulimboka.
Albanie hakutaka kuweka wazi ni nini hasa ambacho atakwenda kuzungumzia kuhusu Dk Ulimboka bali alisisitiza kuwa taasisi yake itazungumzia suala hilo la kutekwa na kipigo cha daktari huyo.
Chanzo:This Day Magazine

0 comments: