Subscribe:

search

.

Tuesday 21 August 2012

RIPOTI KAMILI YA HUKUMU ILIYOMVUA MADARAKA DK KAFUMU HII HAPA


 


Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, leo imetengua ushindi wa kiti cha Ubunge wa jimbo la Igunga, Tabora kilichokuwa kinakaliwa na Dkt. Dalaly Peter Kafumu (CCM), baada ya kuridhika na hoja 8 kati ya 15 zilizowasilishwa na upande wa mlalamikaji.

Dkt. Kafumu anatakiwa kulipa gharama zote za kuendesha kesi na anayo ruhusa ya kukata rufaa ikiwa hakuridhika.
Kesi dhidi ya matokeo ya uchaguzi huo ilifunguliwa na aliyekuwa mgombea wa kiti hicho kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mwalimu Joseph Kashindye akiwashitaki Dkt. Kafumu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema na aliyekuwa Msimamizi wa Uchaguzi jimboni humo, Bw. Protace Mgayane akiwashitaki kuwa wakati wa kampeni, watuhumiwa walitoa vitisho, ahadi ya ujenzi wa Daraja la Mbuntu na kugawa mahindi.

Shauri hilo lilianza kusikilizwa Machi 26, mwaka huu na Jaji Mery Nsimbo Shangali.

Kabla ya uchaguzi uliompa Dkt. Kafumu ushindi, kiti hicho kilikuwa kinashikiliwa na Rostam Aziz (CCM) ambaye alijiuzulu wadhifa huo kwa sababu binafsi.

Akizungumza na gazeti la Majira kwa njia ya simu, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Nzega, Silvester Kainda, alisema awali Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, ilipanga kutoa hukumu Agosti 20, mwaka huu lakini kwa bahati mbaya siku hiyo ilikuwa ni sikukuu hivyo ikaahirishwa hadi leo.

Wakili wa Mlalamikaji Profesa Abdallah Safari, alisema zaidi ya malalamiko 13 waliyawasilisha mahakamani.

Gazeti la HabariLeo limeandika kuwa, katika kesi hiyo baadhi ya mawaziri, akiwamo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu, Stephen Wasira na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba walitoa ushahidi. Wengine ni Mweka Hazina wa CCM, Mwigulu Nchemba na Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Rage.

Waziri Simba akiwa shahidi wa 16 kwa upande wa mshitakiwa alitoa ushahidi wa kula chakula na wanachama wa CCM katika Hospitali ya Nkinga Kata ya Inkiga. Alikiri kula na watu zaidi ya 50 hali ambayo mawakili wa mlalamikaji waliendelea kumhoji wakihusisha maneno aliyotamka kuwa ‘msimchague Kashindye kwani hana mke pia ni masikini’, hata hivyo Waziri huyo alikanusha kutoa kauli hiyo.

Akiwa shahidi wa 15 upande wa washitakiwa, Rage alikiri kushiriki kampeni hizo za uchaguzi akipangiwa kata za tarafa ya Igulubi. Wakili wa mlalamikaji alimhoji shahidi huyo juu ya umiliki wa bastola na kwa nini alikuwa nayo katika mikutano ya kampeni ambayo alishiriki. Rage alikiri kumiliki bastola na kuwa nayo katika shughuli nzima za kampeni wakati huo. Hata hivyo, alisema upepo ulimponza ulipopeperusha shati lake na bastola hiyo kuonekana hadharani na vyombo vya habari kumpiga picha sawia.

www.wavuti.com

0 comments: