Subscribe:

search

.

Saturday 18 August 2012

WABUNGE WAMKATALIA SPIKA ANNE MAKINDA KUWAZIBA MDOMO

 

Boniface Meena
WABUNGE wamemkatalia Spika, Anne Makinda kuwaziba mdomo kuhusu kuzungumzia tuhuma za rushwa zinazowakabili baadhi yao wakiwa majimboni. Wakizungumza baada ya kauli hiyo ya Spika Makinda, wabunge hao walisema hawaoni mantiki ya kuzuiwa kuzungumzia suala hilo wakati ufisadi ni moja ya matatizo ya kitaifa.

Juzi, Spika Makinda wakati akiahirisha Mkutano wa Nane wa Bunge, aliwazuia wabunge kujadili wakiwa majimboni, tuhuma za rushwa zinazowakabili baadhi yao zilizoibuliwa wakati wa Bunge hilo la Bajeti.

Spika alitoa msimamo huo kama mwongozo, baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutoa hoja ya kuliahirisha Bunge hadi Novemba, mwaka huu. Alisema ni muhimu wabunge wakaacha kulijadili suala hilo wakiwa majimboni kwa kuwa bado linafanyiwa kazi na kamati ndogo inayoongozwa na Hassan Ngwilizi.

“Napenda kuwasihi waheshimiwa wabunge msiende kuzungumzia masuala ya rushwa kwenye majimbo yenu, kamati iliyoundwa ni quasi judicial (mahakama ndogo), hivyo ina nguvu ya kimahakama,” alisema Spika Makinda. Alisema ameiongezea muda kamati hiyo ndogo hadi Septemba 14, mwaka huu kumaliza kazi yake.

“Nimesema msilizungumzie kwa sababu kuna baadhi ya magazeti pia yatahojiwa kwa sababu tayari yamekuwa yakiandika taarifa ambazo haijulikani zimetoka wapi,” alisema Spika Makinda.

Maoni ya wabunge
Baadhi ya wabunge wamekuwa na maoni tofauti kuhusu msimamo huo wa Spika. Mbunge wa Musoma Mjini (Chadema), Vicent Nyerere alisema hatua hiyo ni kuwafunga mdomo wabunge wanaochukia rushwa ili wasiendelee kuikemea. “Watoaji na wapokeaji rushwa hawataiacha tabia ya rushwa, siyo kwa kuwa wana nguvu kubwa ila kwa kuwa wanaoichukia rushwa wananyamazishwa,” alisema Nyerere. Alisema wito huo wa Spika Makinda hautekelezeki kwani wananchi majimboni lazima watawauliza wabunge wao kuhusu tuhuma hizo zilizowakumba baadhi ya wabunge na kusababishwa kuvunjwa kwa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini.

Mbunge wa Ludewa (CCM), Deo Filikunjombe alisema wabunge kusemana wenyewe ni jambo jema katika mapambano dhidi ya rushwa. “Bunge halijachafuka kwa suala hilo lakini kilichotokea ni hatua njema ya kupata Bunge zuri hapo baadaye, tumejisema wenyewe ili kujiangalia,” alisema Filikunjombe.

Filikunjombe alisema hata Sheria ya Rushwa inayolalamikiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah kuwa inamzuia kuwafikisha wala rushwa wakubwa mahakamani mpaka apitie kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), inawezekana iko hivyo kwa ajili ya kulindana.

Kwa upande wake, Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed alisema haoni kama kuna tatizo kwa mbunge yeyote kuzungumzia suala la rushwa kwa ujumla, kitu muhimu ni kutokutaja majina ya watu.

Alisema jambo muhimu ni kuwa yale madai yaliyoko kwenye kamati yasizungumziwe kwani kufanya hivyo ni tatizo kwa wale ambao wanatuhumiwa. “Wengine wanaweza kutumia majukwaa kujisafisha na tuhuma hizo wakati bado kamati inaendelea na uchunguzi wake kitu ambacho si sawa kwenye mwenendo wa kazi za Mahakama,” alisema Rashid.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Ester Bulaya alisema wabunge wana akili na kwamba hawawezi kuacha kuzungumzia masuala ya rushwa kwa kuwa wanazijua kanuni na taratibu za kisheria zilivyo.

Alisema wabunge lazima waendelee kuikemea rushwa kwa nguvu zote kwani kuna namna ya kuzungumzia masuala hayo bila kuingilia ushahidi wa kamati inayochunguza.
“Sioni kama kuzungumzia masuala ya rushwa kuna tatizo, wabunge ni watu wazima na wanaelewa mipaka yao hivyo sidhani kama wataingilia kazi za kamati ,”alisema Bulaya.

Kamati inayoendesha uchunguzi huo inaongozwa na Mbunge wa Mlalo, Brigedia Jenerali Mstaafu, Hassan Ngwilizi. Wajumbe wake ni John Chiligati (Manyoni Magharibi), Riziki Omar Juma (Viti maalumu), Said Amour Arfi (Mpanda Mjini) na Gosbert Blandes (Karagwe).
Chanzo:Mwananchi.co.tz

0 comments: