Subscribe:

search

.

Wednesday 10 October 2012

MAKAMU WA RAIS AIWAKILISHA TANZANIA UHURU WA UGANDA



Uganda ilipata uhuru wake Oktoba 09, mwaka 1962 na jana Jumanne 09 Oktoba, 2012 iliadhimisha miaka 50 ya uhuru huo katika sherehe zilizofanyika katika uwanja wa Mapinduzi wa Kololo na kuhudhuriwa na Mwenyeji wa Sherehe hizo Rais Yoweri Kaguta Museveni. 

Sherehe hizo za aina yake zilipambwa na vikosi mbalimbali vya kijeshi vilivyopita mbele ya Amiri Jeshi Mkuu Rais Museveni na kutoa heshima zao za utii kwa kiongozi huyo, sambamba na vikundi mbalimbali vya burudani ambavyo vilitumbuiza wakati wote wa sherehe, huku wananchi mbalimbali wa Uganda ambao hawakupata nafasi ya kufika katika uwanja wa Kololo wakitazama tukio hilo la kihistoria kupitia televisheni mbalimbali. 

Sambamba na hilo pia vyombo mbalimbali vya kiusalama, vilikuwa vikitumia kila aina ya taarifa sambamba na kuzunguka eneo la maadhimisho wakati wote ili kuhakikisha kuwa sherehe hizo zinafanyika na kumalizika kwa usalama kama ambavyo imetokea.

Sherehe hizi ziliongozwa kwa lugha tatu, ya kwanza ikiwa ni Kiswahili ambacho kilitumika kutoa amri kwa vikosi vya majeshi na hii inadhihirisha wazi kuwa lugha hii imejikita zaidi miongoni kwa wanajeshi wa Uganda, lugha ya Kiganda na Kiingereza. 

Vyombo mbalimbali vya habari vya Uganda vimeelezea kuwa tukio hili la kuadhimisha miaka 50 ya uhuru, ni moja ya matukio makubwa kabisa ambayo yametokea Uganda na ambayo yameonesha kuwa taifa hilo lina kila sababu ya kuunganisha nguvu zake na kubakia taifa moja tofauti na sasa ambapo kuna hali kadhaa za kusigana miongoni mwa wananchi hali inayofanya kukosekana kwa utulivu wa moja kwa moja.   

0 comments: