Subscribe:

search

.

Monday 8 October 2012

BILIONI MBILI KUPELEKA UMEME VIJIJI VYA LINDI NA MTWARA




Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo.
 

Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni mbili kwa ajili ya kufikisha umeme katika vijiji vya mikoa ya Lindi na Mtwara  ikiwa ni mpango wa kufikisha miundombinu ya umeme katika vijiji mbalimbali kwa asilimia therethini nchi nzima  ifikapo mwaka 2015.
Kaimu Meneja wa Shirika la umeme TANESCO Mkoa wa Mtwara  Mhandisi Daniel Kiando amewaambia waandishi wa habari kuwa fedha hizo zimetengwa kwa ajili ya  miradi therathini na moja (31) ambapo vijiji vilivyopo katika wilaya za Masasi, Newala na Tandahimba vitanufaika.
“Mpaka sasa tayari mradi umekamilika kwa asilimia mia moja katika kijiji cha Mbambakofi kilichopo wilaya ya Tandahimba na  wateja wanaendelea kujaza fomu kwa ajili ya kuwekewa umeme katika nyumba zao,” amesema Kiando.
Kiando amefafanua kuwa nyumba zitakazowekewa umeme ni zile ambazo zimeezekwa kwa bati hivyo ametoa wito kwa wananchi kuezeka nyumba zao ili waweze kunufaika na mradi huo pamoja na kurahisha maendeleo yao kwa ujumla.
Nae mkazi wa kijiji hicho Asha Nalamba amesema kuwa amefurahishwa na kitendo cha Serikali kupeleka mradi huo vijijini na tayari ameanza kujipanga kuezeka nyumba yake kwa bati ili aweze kunufaika na umeme huo.
“Mimi nina nyumba ya nyasi lakini tulivyotangaziwa mradi huu, nikaanza polepole kujipanga na mpaka sasa nimeshanunua mabati ishirini, natarajia mwezi Novemba  mwaka huu kuzeeka,” amesema Nalamba.
Hii ni kati ya miradi ambayo wananchi wa Lindi na Mtwara wamepata punguzo la bei ya umeme ambapo kwa sasa wanalipia elfu tisini na tisa tu badala ya laki nne na elfu hamsini na tano na mwisho wa punguzo hili ni mwezi Desemba mwaka huu.

0 comments: