search

.

Wednesday, 10 October 2012

CHADEMA YAIFUNIKA CCM GEITA

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeitikisa ngome ya mbunge wa Jimbo la Busada wilayani Geita, Lorencia Bukwimba baada ya kuzoa wanachama 18,670 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakiwamo wazee na makada maarufu wa chama hicho.

Wanachama hao wamehama kwa wingi wakati CCM ikiwa katika heka heka ya uchaguzi wa viongozi wa nafasi mbalimbali kwenye jumuiya zake. Mbali na kuzoa maelfu ya wanachama wa CCM kwenye jimbo hilo, linalokadiriwa kuwa na wapiga kura zaidi ya 200,000, pia Chadema kimeunda uongozi kwa kuteua wenyeviti, makatibu, na wahazini wa chama kwenye kila kata zilizokuwa hazina uongozi ngazi ya tawi.

Viongozi waliosimikwa ni wenyeviti, makatibu, waenezi na wahazini wa matawi, pamoja na wale wa jumuiya mbalimbali za chama hicho hususani wazee (Bawawacha), vijana (Bavicha) na wanawake (Bawacha) lengo likiwa ni kukiimarisha chama kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kikao cha majumuisho ya ziara yake kwenye jimbo hilo, kilichofanyika kwenye Ofisi ya Chadema ya Wilaya ya Geita, Kiongozi wa M4C mkoani Geita, Alphonce Mawazo alifafanua kuwa, wana CCM waliohamia Chadema wametoka katika kata 13, kati ya 16 za jimbo hilo. Amesema kati yao 11,235 ni wanachama wapya na 7,435 ni waliovua Gamba na kuvaa Gwanda kuunganisha nguvu ili kuhakikisha Chadema kinaibwaga CCM kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na kuingia Ikulu.

Wanachama hao walijiunga na Chadema wakati wa mikutano yake iliyofanyika kwa nyakati tofauti katika kata 13, kati ya 16 za jimbo hilo. wanachama wengine,70 walirudisha kadi za CCM na kujiunga na Chadema ni kutoka katika Kijiji cha Nyabulolo, Kata ya Kamena alipozaliwa mbunge wa sasa wa jimbo hilo kupitia CCM, Rolencia Bukwimba.

Aliwataja miongoni mwa wazee na makada wa siku nyingi wa CCM,walioamua kurudisha kadi za chama hicho na kuhamia Chadema ni pamoja na Thereza Lugembe (79), mkazi wa Kijiji cha Nyabulolo, Kwando Maduhu (109), mkazi wa Kijiji cha Nyarugusu na Shija Mihambo (87), mkazi wa Bugogo Bukoli. “Kazi hii siyo ndogo ndugu waandish, ni kazi kubwa sana, tunapambana na chama ambacho kinamizizi kila kona, tumezoea kuona vijana ndiyo wanajiunga na Chadema, lakini unapoona wazee ambao ndiyo wamekuwa wanahongwa chumvi kwenye chaguzi mbalimbali nao wameanza kukimbia ujue saa ya ukombozi imekaribia,”amesema Mawazo.

0 comments: