search

.

Wednesday, 10 October 2012

MZEE MWINYI ATINGA MAHAKAMANI KISUTU

Rais Mstaafu wa awamu wa pili, Ali Hassan Mwinyi, amekwenda Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kwa ajili ya kutoa ushahidi katika kesi ya wizi wa kuaminiwa wa sh. Milioni 37.44 zinazotokana na pango la nyumba zake baada ya mtu mmoja kutoa maelezo ya udanganyifu kwa Rais huyo mstaafu.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 201/2012 inamkabili mfanyabiashara Abdallah Mzombe (39), mkazi wa Kinondoni Mkwajuni, aliyeaminiwa na Mzee Mwinyi na kupewa kazi ya kukusanya kodi katika nyumba zake mbili zilizopo jijini Dar es Salaam.

Kesi hiyo ipo mbele ya Hakimu Mkazi, Geni Dudu, na upande wa Jamhuri unaongozwa na wakili wa Serikali, Charles Anindo.Hata hivyo waandishi wa habari hawakuruhusiwa kuingia katika chumba cha hakimu kusikiliza kesi hiyo. “Amekuja mahakamani kutoa ushahidi katika kesi hiyo, upande wa Jamhuri bado haujafunga ushahidi,” amesema mmoja wa mawakili wa Serikali aliyefuatwa na waandishi wa habari kutaka kujua kwanini Mzee Mwinyi yupo katika mahakama hiyo.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Mzombe anakabiliwa na makosa mawili ya wizi wa kuaminiwa wa Sh milioni 37.44. Katika tarehe tofauti, kati ya Januari Mosi, mwaka jana na Julai 10, mwaka huu, katika eneo la Mikocheni, Wilayani Kinondoni,Dar es Salaam, akiwa ni wakala wa Mzee Mwinyi, Mzombe aliiba Sh. Milioni 17. 64 baada ya kukusanya kodi ya nyumba namba 481 iliyopo Mikocheni ‘A’ Hati ya mashtaka inaeleza kwamba kodi hiyo ni mwaka 2011/2012 na 2012/2013 na katika shtaka la pili, Mzombe anadaiwa katika tarehe hizo, katika eneo la Msasani Village, Konondoni akiwa wakala wa Mwinyi aliiba Sh milioni 19.8 zinazotokana na makusanyo ya kodi ya nyumba namba 55, katika mwaka 2011/2012 na 2012/2013. Kesi hiyo itasikilizwa Oktoba 22, mwaka huu.

Ifuatayo ni sehemu ya maswali jkati ya ofisa usalama na waandishi wa habari ambao walikuwa wakitaka kuingia ndania ya chumba cha mahakama. Ofisa Usalama: Mnakwenda wapi? Waandishi: Tunakwenda mahakamani. Ofisa Usalama: Ninyi ni kina nani? Waandishi: Waandishi wa habari. Ofisa Usalama: Mmeambiwa kuna mahakama hapa? Waandishi: Ndiyo, hii ni mahakama. Baada ya kujibiwa hivyo, ofisa usalama huyo alinyoosha mkono kuzuia wasiingie ndani huku akisema: “Hii haiwahusu”.! Mzee Mwinyi alitoka Mahakamani saa 6:24 mchana na kupanda gari lenye namba gari yake na kuondoka. 

0 comments: