Subscribe:

search

.

Tuesday 9 October 2012

MAKAMU WA RAIS AIWAKILISHA TANZANIA, MKUTANO WA MAZIWA MAKUU, UGANDA.

Mheshimiwa Makamu wa Rais na ujumbe wake umewasili nchini hapa salama na moja kwa moja kushiriki kupata taarifa za mikutano ya ngazi ya Mawaziri ambapo Tanzania iliwakilishwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Omari Juma Mahadhi. Katika mazungumzo hayo ya awali, Mheshimiwa Waziri Vuai alimueleza Mheshimiwa Makamu wa Rais kuwa, Tanzania inabakia kuwa na sifa yake ya siku zote ya kuthamini na kujitoa kusaidia kupatikana kwa amani katika nchi zinazoizunguka sambamba na zile zinazohitaji msaada wake. Akifafanua kuhusu makubaliano katika ngazi ya Mawaziri, Waziri Vuai alimhakikishia Mheshimiwa Makamu wa Rais kuwa Tanzania imewakilishwa vizuri na kwamba nchi nyingine wanachama zinategemea sana mchango wa Tanzania katika kuisaidia Congo (DRC) kufikia amani ya kudumu na hivyo wananchi wake kuendelea na shughuli za kunyanyua vipato vyao bila hofu ya usalama wa maisha yao. Kwa upande wake Mheshimiwa Naibu Waziri Mahadhi alimueleza Mheshimiwa Makamu wa Rais kuhusu ushiriki wa Tanzania katika nchi za Maziwa Makuu na akafafanua kuwa nchi hizi zinategemeana sana katika hali mbalimbali za maisha hivyo Tanzania bado inayo fursa nzuri ya kuendeleza mahusiano na nchi hizi kwa angalizo kubwa la kutazama fursa za kiuchumi. Katika mkutano huo wa wakuu wa nchi uliofanyika katika eneo la Munyonyo nje kidogo ya jiji la Kampala, Wakuu na Wawakilishi wa wa nchi mbalimbali, walikutana majira ya saa tano na kisha mwenyeji wa Mkutano huo, Rais Yoweri Kaguta Museveni kuufungua. Rais Museveni alitumia nafasi hiyo, kuwashukuru viongozi wote akianza na Rais wa Rwanda Paul Kagame ambaye alimpongeza kutokana na ushiriki wake katika mazungumzo ya kufanikisha amani Congo (DRC) na kisha akamshukuru Rais Joseph Kabila wa Congo (DRC) kwa kukubali kuzieleza nchi wanachama wa nchi za Maziwa Makuu kuhusu hali mbaya ya kiusalama nchini kwake na kukubali kutaka msaada kutoka kwa nchi hizi. Mjadala mkubwa katika mkutano huu ulikuwa kuhusu kuundwa kwa jeshi lisilofungamana na upande wowote ili lisaidie kumaliza mapigano katika Congo (DRC) na kisha kuiwekea nchi hiyo misingi ya kuwa na amani ya kudumu. Mkutano huu pia ulihudhuriwa na Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir ambaye alikuja na hoja ya kutaka nchi yake iharakishiwe nafasi ya uanachama katika umoja huu, jambo ambalo baadhi ya nchi limeona ni bora, lakini zikatoa angalizo kuwa lazima nchi hiyo licha ya kuwa na nia na sifa ya kuwa mwanachama, ifuate utaratibu wa kawaida wa kutafuta nafasi ya uanachama na sio kuruka taratibu. Mkutano huu unafanyika nchini Uganda wakati nchi hii ikijitayarisha kuadhimisha sherehe za miaka 50 ya uhuru wake, huku hali vya usalama nchini hapa vikionesha kila sababu ya kulinda amani katika tukio hili nyeti katika historia ya Uganda na Afrika Mashariki. IMETOLEWA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS , KAMPALA, UGANDA:

0 comments: